Trafiki matatani kwa madai ya kudhalilisha Jeshi la Polisi

Dar es Salaam. Askari wa usalama barabarani walioonekana wakichukua rushwa kutoka kwa madereva wa daladala, wamekamatwa na Jeshi la Polisi.

Video iliyosambaa mitandaoni leo Januari 15, imewaonyesha askari hao, mmoja wa kike na mwingine wa kiume wakipokea vitu vinavyodhaniwa kuwa fedha kutoka kwa madereva wa daladala zilizosimamishwa na kisha kuwaruhusu waondoke eneo la Vingunguti, Dar es Salaam.  

Akizungumza leo Jumatano Januari 15, 2024 na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema tayari wamewakamata polisi hao na wapo mahabusu.

Muliro amesema wamewakamata askari hao kwa kuwa wamefanya vitendo visivyo vya maadili ambavyo vinachafua taswira ya Jeshi la Polisi.

“Kwenye picha ile wanaonekana askari wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume, wakati wa kutekeleza majukumu yao wakifanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili  na Jeshi la Polisi na kuchafua taswira ya Jeshi na Serikali kwa ujumla.

“Askari hao tayari wamekamatwa, wapo mahabusu na hatua kali za kinidhamu za mashtaka ya kijeshi zimeanza kuchukuliwa kabla ya hatua nyingine za kisheria dhidi yao zitakazoamuliwa kuchukuliwa,” amesema Muliro bila kuwataja majina.

Aidha, Kamanda Muliro amesema jeshi hilo halitavumilia vitendo vyovyote vya kulidhalilisha au kwenda kinyume nalo.

Related Posts