Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema watoto wawili waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha wakiwa na mfanyakazi wa ndani siku tano zilizopita wamepatikana.
Imeelezwa katika taarifa ya polisi kuwa watoto hao wamepatikana wakiwa kwa mganga wa kienyeji Kimara Baruti, jijini Dar es Salaam.
Watoto hao, wakazi wa Tandika, jijini Dar es Salaam, ni Husna Gulam mwenye miaka mitatu na Mahdi Mohamed (4).
Taarifa za kutoweka watoto hao siku tano zilizopita zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, mama yao akipaza sauti kuomba msaada kuwezesha wapatikane.
Akizungumza leo Jumatano, Januari 15, 2024, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema watoto hao wamepatikana jana Januari 14, 2025, wakiwa Kimara.
Amesema watoto hao waliibwa nyumbani kwao Tandika, jijini Dar es Salaam, na mfanyakazi huyo wa ndani kwa kushirikiana na mganga huyo wa kienyeji, Abdulkarim Shariff (43).
“Watoto hao wamepatikana Januari 14, 2025, nyumbani kwa mganga huyo Kimara Baruti, jijini Dar es Salaam. Walipelekwa hospitali haraka kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na hawajakutwa na tatizo lolote,” amesema.
Kwa mujibu wa Muliro, baba mzazi wa watoto hao, Mohamed Kassim, amesema mfanyakazi wa kazi za ndani ambaye bado hajakamatwa waliishi naye nyumbani kwa siku nne tu, hivyo ilikuwa ngumu kutambua kama anaweza kuwa na dhamira mbaya.
“Mahojiano ya kina na watuhumiwa yanakamilishwa kubaini nini kiini na malengo ya tukio hilo. Watafikishwa kwenye mamlaka nyingine za kisheria haraka iwezekanavyo kwa hatua zaidi,” amesema.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuepuka tabia ya kuchukua wasaidizi wa kazi za nyumbani wasiojua historia na tabia zao ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea.