Ukraine yaishambulia Russia kwa makombora Storm Shadow, ATACMS

Kyiv. Jeshi la Ukraine limefanya mashambulizi mazito usiku wa kuamkia leo nchini Russia, kwa kutumia droni zaidi ya 100 na makombora yaliyotengenezwa nchini Uingereza ya Storm Shadow na ATACMS ya Marekani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Russia Today, mashambulizi hayo ya kushtukiza yamefanyika tangu Russia itangaze kuanza operesheni zake nchini Ukraine usiku wa kuamkia leo Jumatano Januari 15, 2025. 

Mashambulizi hayo yamefanyika zikiwa zimebaki siku nne kufikia uapisho wa Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump, ambaye kipaumbele chake atakapoingia ikulu ya taifa hilo ni kukomesha vita hiyo.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imeandika kupitia akaunti yake ya mtandao wa Telegram kuwa italipiza vikali mashambulizi hayo ya Ukraine yaliyolenga eneo la Jiji la Saratov na Engels nchini Russia.

Jeshi la Russia limesema makombora mengi yalidhibitiwa na mfumo wa kujilinda wa anga nchini humo huku mengine yaliyopenya na kupiga maeneo yaliyolengwa yakidhibitiwa kuleta madhara kwa raia hususan ni maeneo hayo yenye miundombinu ya viwanda.

Taarifa zinadai kuwa sehemu ya viwanda eneo la Jiji la Saratov na Engels vimeharibiwa vibaya na makombora hayo huku baadhi ya shule zikilazimika kusitisha vipindi leo kutokana na tishio la kufanyika shambulizi lingine.

Eneo hilo lilishambuliwa na Jeshi la Ukraine wiki iliyoisha, ambapo shambulizi hilo lililenga na kupiga kiwanda ambacho ni hifadhi ya mafuta ambayo ni tegemeo kwa ajili ya ndege za kijeshi za Russia.

Moto uliosababishwa na shambulizi hilo ulizimwa muda mfupi baada ya shambulizi hilo kufanyika huku madhara yake yakifichwa.

Jeshi la Ukraine lilisema jana pia kuwa linalenga kushambulia Jimbo la Bryansk, Tula na Tatarstan, maeneo hayo ni mashuhuri kwa kuwa na viwanda vya kemikali na utengenezaji wa silaha za kivita.

Ukraine imekuwa ikitumia silaha na makombora ya ATACMS iliyopewa na Marekani na Storm Shadow iliyopewa na Uingereza Novemba mwaka 2024 kushambulia maeneo yenye miundombinu ya nishati nchini Russia.

Kwa upande wake Urusi, imekuwa ikionya matumizi ya silaha hizo kwa kile ambacho inadai kufanya hivyo ni kuilazimisha kujibu mapigo kwa kushambulia kwa kutumia makombora yake ya masafa ya kati aina ya Oreshnik.

Urusi ambayo hadi sasa imeyakamata maeneo mbalimbali ya Ukraine ikiwemo ya Mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Pokrovisk, na Crimea iliyotwaliwa mwaka 2014, imekuwa ikisisitiza kuwa iko tayari kwenda kwenye meza ya mazungumzo isipokuwa masharti yake yatakapotimizwa na Ukraine.

Masharti hayo ni pamoja na Ukraine kuacha matumizi ya silaha ilizopewa na Marekani kuishambulia Russia, Rais Volodymyr Zelenskyy kuitisha uchaguzi utakaomuweka madarakani kihalali huku ikisema Rais huyo yupo madarakani kwa nguvu ya Sheria ya Kijeshi (Martial Law).

Pia Russia inaitaka Ukraine kuachana na msimama wake wa kutaka kujiunga na Jumuiya ya Kujilinda ya Nato.

Katibu Mkuu wa Nato, Mark Rutte akizungumza jana alisema Ukraine haiko katika nafasi nzuri ya kukubaliana na masharti hayo na kusema kuwa uamuzi huo utategemea msimamo wa Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump.

Trump alisema akiapishwa kuingia Ikulu ya White House atahakikisha anaumaliza mzozo huo ndani ya saa 24 kabla ya wateule wake hususan ni Keith Kellogg kudai kuwa Rais huyo ataumaliza mzozo huo ndani ya kipindi cha siku 100 tangu kuingia ikulu.

Hata mwanadiplomasia wa Marekani, William Courtney alisema Rais huyo anayekwenda kuingoza Marekani kwa awamu nyingine ataweza kulifanikisha hilo ndani ya siku 100 na siyo saa 24 kama alivyoahidi awali.

“Nadhani kutabiri kuwa mzozo huo utamalizwa ndani ya saa 24 ni suala gumu na lisilotimizika kwa sababu hakuna anayejua kuwa mazungumzo kati ya pande hizo yatakwenda vipi,” amesema Courtney.

Courtney amesema mashambulizi mfululizo ya Ukraine nchini Urusi siku za hivi karibuni yanaweza kutuma ujumbe kwa Trump kuwa mapigano hayo yanaweza kuendelezwa hata bila misaada ya Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.

Wakati Ukraine ikiendesha mashambulizi hayo, vikosi vya Urusi vinaendelea kuyateka maeneo ya ndani ya Mashariki mwa Ukraine hususan ni kuukaribia Mkoa wa Kiev, ambapo ni makao makuu ya nchi hiyo na kuimarisha ulinzi wake eneo la Kursk ambako walikamatwa wanajeshi wawili wa Ukraine.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts