MSHAMBULIAJI Abdoulaye Yonta Camara ameungana na nyota wengine kutoka Singida Black Stars kuitumikia Pamba Jiji kwa mkopo wa miezi sita.
Nyota waliotua Pamba Jiji katika dirisha dogo la usajili ambalo lilifungwa jana usiku kutoka Singida Black Stars ni pamoja na Habib Kyombo, Hamad Majimengi na Mohamed Kamara.
Taarifa kutoka Singida BS zimethibitisha kumuondoa mchezaji huyo na kumpeleka Pamba Jiji kwa mkopo wa miezi sita akiungana na nyota wengine watatu kufanya idadi kuwa wachezaji wanne.
Msemaji wa Pamba Jiji, Moses William alisema ni kweli wamekamilisha usajili wa wachezaji wanne sasa kutoka Singida Black Stars na wanaamini ongezeko lao litakuwa chachu ya mafanikio kikosini mwao.
“Yonta ni usajili ambao ulichelewa kidogo tofauti na kina Kyombo ambaye tayari ameshaanza kuitumikia timu tuna imani kubwa na wachezaji hao tuliowapata na tunaamini kikosi chetu kitakuwa shindani mzunguko wa lala salama.”
Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza alisema wamepeleka wachezaji wanne Pamba Jiji na wote wanaamini watakwenda kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na uwezo walionao.
“Kuwatoa wachezaji hao kwa mkopo haina maana kwamba hawana uwezo wa kuanza kikosi cha kwanza timu nyingine ni wachezaji wazuri, lakini ushindani uliopo kwenye kikosi chetu sasa umewanyima nafasi ya kucheza,” alisema Masanza.