Dar es Salaam. Kesi ya mauaji inayomkabili Sophia Mwenda anayedaiwa kumuua binti yake akishirikiana na kijana wake wa kiume, imerejeshwa tena kwa Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga kuisikiliza kwa niaba ya Mahakama Kuu, badala ya Jaji.
Hii ni mara ya pili Hakimu Kiswaga ambaye ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu kupangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu Kiswaga ni mmoja wa mahakimu wakazi wenye mamlaka ya ziada, yanayowawezesha kusikiliza kesi za jinai ambazo kwa mujibu wa Sheria zinapaswa kusikilizwa na Jaji, Mahakama Kuu, zikiwemo za mauaji kama hii.
Awali kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya hatua ya uchunguzi wa awali, kwa mujibu wa sheria ili kukamilisha taratibu za awali ikiwemo upelelezi, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji na uamuzi.
Washtakiwa hao Sophia Mwenda na kijana wake, Alphonce Magombola wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya mwanafamilia Beatrice Magombola, Desemba Mosi, 2020, eneo la Kijichi, wilayani Temeke, Dar es Salaam.
Walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza Julai 15, 2022 na kusomewa shtaka hilo.
Katika hatua hiyo ya uchunguzi wa awali ilisikilizwa na Hakimu Kiswaga na baada ya hatua hizo ukiwemo upelelezi kukamilika, Julai 23, 2023, washtakiwa walisomewa maelezo ya mashahidi na kwa hatua hiyo Mahakama ya Kisutu ilihitimisha jukumu.
Hivyo siku hiyo Mahakama hiyo ilifunga jalada la kesi hiyo mahakamani hapo na ikatoa amri ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutolea hukumu, kama sheria inavyoelekezwa.
Hata hivyo, ilirejeshwa kwa Hakimu Kiswaga kwa ajili ya kuisikiliza na kuiamua, kulingana na mamlaka ya ziada aliyo nayo.
Desemba 16, 2024, kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (washtakiwa kusomewa hoja za awali na kisha kutakiwa kubainisha mambo wanayokubaliana nayo na yale wale wasiyokubaliana nayo) kabla ya kuanza kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo, siku hiyo mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali Asiath Mzamiru, aliieleza Mahakama kuwa wasingeweza kuendelea kwa kuwa jalada la kesi hiyo wamelirejesha Mahakama Kuu ili ipangiwe Jaji wa kuisikiliza.
“Kwa leo tutashindwa kuendelea kwa sababu tunasubiri re-assignment (kupangiwa Jaji wa kuisikiliza) Mahakama Kuu”, alisema Wakili Mzamiru na akaomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuangalia kama itakuwa imeshapangiwa Jaji wa kuisikiliza.
Hoja hiyo haikupingwa na wakili wa washtakiwa Denis Mniko, ambaye aliieleza Mahakuwa hana pingamizi na Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo akaipanga Desemba 30, 2024, kutajwa kuona kama ingekuwa imeshapangiwa Jaji wa kuisikiliza na kuiamua.
Baadaye alipoulizwa na Mwananchi sababu ya hatua hiyo, Mzamiru alifafanua kuwa mabadiliko hayo yametokana na aina ya ushahidi wa kesi hiyo.
“Unajua hii ni kesi ya mauaji, Mahakama Kuu ndio yenye mamlaka ya kusikiliza kesi kama hizi lakini wakati mwingine hakimu mwenye mamlaka ya ziada anaweza kupangiwa kuisikiliza”, alisema na kufafanua zaidi:
“Lakini kwa aina ya ushahidi wa kesi hii tumeona sisi hatuwezi kuisikiliza, hivyo tumeirudisha mahakama Kuu ipangiwe jaji wa kuisikiliza.”
Desemba 30, 2024 ilipotajwa bado ilikuwa haijapangiwa jaji, hivyo ikaahirishwa mpaka leo, Januari 15, 2025.
Baadaye kesi hiyo ilirejeshwa tena kwa Hakimu Kiswaga kuendelea na usikilizwaji.
Hivyo leo Januari 15, 2025 ilitarajiwa kuendelea kwa kuanza na hatua ya usikilizwaji wa awali na kisha kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa ushahidi, lakini imeahirishwa kutokana na Wakili wa mshtakiwa wa pili kutokuwepo.
Wakili Mniko anayemtetea mshtakiwa wa kwanza (Sophia) amesema Wakili wa mshtakiwa wa pili amespata dharura lakini ameelekeza kesi iendelee hata bila yeye kuwepo.
Hata hivyo, hoja hiyo imepingwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Chalo, akiomba iahirishwe ili mshtakiwa huyo apate uwakilishi, kwa tarehe ambayo Wakili wa mshtakiwa wa pili atakuwepo.
Hakimu Kiswaga amekubaliana na hoja ya upande wa mashtaka ana ameahirisha kesi hiyo mpaka Januari 23, 2025, kuendelea na hatua hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi katika tukio hilo, Alphonce alimfunga miguu dada yake Beatrice na kumshikilia mikono kisha mama yake, Sophia akamchomachoma bintiye wa kumzaa, kwa kisu kwenye titi la kushoto mpaka alipofariki dunia.
Kulingana na ushahidi huo, washtakiwa hao walitenda kosa hilo kwa kuwa mwanafamilia huyo alitaka kwenda kutoa ushahidi kwenye kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa hao.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Machi 16, 2020 majira ya saa 4 asubuhi, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kinondoni Ramadhani Kingai, kwa sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), alipokea taarifa kutoka kwa msiri kuhusu kupotea kwa Beatrice Magombola.
Msiri huyo alidai kuwa kumekuwa na taarifa za utata kuhusu kupotea kwake kwani mama mzazi wa Beatrice, Sophia (mshtakiwa wa pili), anadai kuwa mtoto wake amekwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine akiulizwa anadai ameenda nchini Canada kutibiwa.
Hata hivyo, mama huyo hakuweka wazi ugonjwa unaomsumbua Beatrice na taarifa za ugonjwa hazikuwa zikifahamika kwa ndugu wa Beatrice wala baba yake mzazi isipokuwa kaka yake mkubwa Alphonce, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza.
Msiri huyo alieza kuwa, Beatrice alikuwa na gari aina ya Vanguard lililokuwa likitumiwa na Alphonce na pia nyumba yake iliuzwa na Sophia na kwamba kuna wakati washtakiwa hao wakihojiwa kupotea kwa Beatrice wanakuwa wakali.
Kutokana na taarifa hizo za msiri, RPC Kingai alielekeza kufunguliwa jalada la uchunguzi na upelelezi ulifanyika na kufanikiwa kukamatwa kwa washtakiwa hao.
Washtakiwa katika maelezo yao ya onyo wanadaiwa kuwa walikiri kumuua Beatrice kwa kumchoma kwa kisu katika titi la kushoto, baada ya Alphonce kumfunga miguu na kumshika mikono kisha Sophia akamchoma kwa kisu hadi alipofariki.
Baada ya kumuua washtakiwa waliuzungusha mwili wa Beatrice kwa shuka na mkeka na kwenda kuutupa eneo la Zinga, Bagamoyo.
Walieleza kuwa walimuua Beatrice kwa sababu alikuwa anataka kwenda kutoa ushahidi mahakamani Mbeya katika kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa hao.
Baada ya maelezo hayo upande wa mashtaka ulieleza kuwa unatarajia kuwaita mashahidi 40 akiwemo DCI Kingai, na kwamba utawasilisha vielelezo 13.