Baresi, Lyanga kuna siri nzito

BAADA ya kukamilisha usajili wa Danny Lyanga, kocha mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ amefichua siri iliyomfanya amsajili mshambuliaji huyo mkongwe akisema ni uzoefu mkubwa alionao anaoamini utaibeba timu katika duru la pili la Ligi Kuu Bara.

Lyanga aliyekuwa JKT Tanzania, amewahi pia kucheza Tanzania Prisons, Geita Gold, Azam, Simba na  Fanja ya Oman ametua Mashujaa katika dirisha dogo la usajili linalofungwa leo usiku.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baresi alisema usajili umefanyika kutokana na ripoti yake ilivyokuwa inataka kuongezwa mshambuliaji na ujio wa Lyanga anaamini utakuwa na chachu hasa eneo hilo kutokana na uzoefu alionao.

“Kwenye ripoti yangu niliomba kuongezewa mchezaji anayecheza nafasi hiyo. Nafurahi uongozi umefanya kama nilivyotaka kilichobaki ni mimi kutoa maelekezo kwenye uwanja wa mazoezi ili wachezaji wanipe kile nataka,” alisema Baresi na kuongeza:

“Eneo la ushambuliaji lilikuwa tatizo sio kwamba waliopo hawana uwezo, lakini kuna baadhi ya wachezaji hawajacheza zaidi ya mechi sita kati ya 15 za mzunguko wa kwanza kutokana na kusumbuliwa na majeraha mfano Emmanuel Mtumbuka.”

Baresi alisema kuongezwa kwa Lyanga kikosini kwake kutaongeza ushindani na kila mchezaji atatamani kuanza katika mechi, hivyo anaamini eneo hilo litakuwa na chachu tofauti na mzunguko wa kwanza.

Mashujaa kwenye mechi 16 ilizocheza hadi sasa imefunga mabao 14 na kuruhusu nyavu kutikishwa mara 14, hivyo ni wastani wa kwamba kwenye kila mchezo wamekuwa wakiruhusu nyavu kutikishwa.

Related Posts