Asubuhi ya Jumatatu , anga la Gaza lilikuwa limetanda moshi kutokana na mashambulizi ya mabomu na mizinga yaliyofanywa na jeshi la Israel, wakati likijaribu kujipenyeza ndani ya mji wa kusini wa Rafah kwa kile msemaji wake, Daniel Hagari, alichokiita kuwa ni “operesheni maaluum”, na kuwafanya wakimbizi wa ndani wa Kipalestina kukimbia huku na kule kutoka kwenye eneo awali lilikuwa hifadhi yao ya mwisho.
Jeshi la Israel linadai kuwa mji huo ulio mpakani mwa Gazana Misri ni “ngome ya mwisho ya wapiganaji wa Kipalestina” na kwamba lazima likamilishe operesheni yake ya kuwamaliza wapiganaji hao na kuwakombowa mateka waliosalia mikononi mwao.
Soma zaidi: Jeshi la Israel lakabiliana na kundi la wanamgambo la Hamas
Usiku wa Jumapili, jeshi hilo lilikivamia kitongoji cha Zaitun ambako lilidai kuwauwa wapiganaji kadhaa wa Kipalestina.
Wapalestina wapatao 300,000 kati ya raia milioni moja wanaojihifadhi huko, washameukimbia tayari mji huo kufuatia amri iliyotolewa na Israel.
“Hatujuwi wapi tuelekee. Tumekuwa tukikimbia kutoka mahala pamoja kwenda kwengine. Na sasa tumeondoka Rafah, lakini hatujui twende wapi. Tunakimbiakimbia tu mitaani. Nimeona kwa macho yangu. Nimeviona vifaru na matingatinga ya majeshi ya Israel. Yapo mitaani.” Alisema Umm Jumma, mmoja kati ya wakimbizi hao wa ndani.
Wapiganaji wa Kipalestina waendelea na kupambana
Usiku wa Jumapili, jeshi la Israel pia liliushambulia upande wa kaskazini katika kambi ya Jabalia, ambako wapiganaji wa Hamas wamejikusanya tena kwenye maeneo ambayo jeshi hilo liliwahi kudai kuwa lilishayasafisha miezi kadhaa iliyopita.
Jeshi hilo lilisema liliwauwa pia wapiganaji kadhaa wa Kipalestina kwenye operesheni hiyo.
Hamas, inayotambuliwa na mataifa kadhaa na Magharibi kuwa kundi la kigaidi, ilisema kwenye taarifa yake ya Jumapili kwamba wapiganaji wake walishambuliana na jeshi la Israel kwenye upande wa mashariki wa kambi hiyo ya Jabalia.
Soma zaidi: Israel: Mapambano yanaendelea mashariki mwa mji wa Rafah
Vidio iliyotolewa na tawi la kijeshi la kundi hilo, al-Qassam Brigades, ilionesha wapiganaji wake wakirusha droni iliyodondosha mabomu kwenye kifaru cha Israel karibu na kambi hiyo.
Taarifa ya al-Quds, ambalo ni tawi la kijeshi la Islamic Jihad, ilisema kwamba wapiganaji wao walipambana na wanajeshi wa Israel mashariki mwamji wa Rafah.
Ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jeshi la Israel limewauwa Wapalestina 63 na kuwajeruhi wengine 114, na hivyo kuifanya idadi ya vifo kufikia 35,034 na majeruhi 78,755 tangu awamu ya sasa ya mapigano ilipoanza tarehe 7 Oktoba, kufuatia uvamizi wa wanamgambo wa Kipalestina dhidi ya Israel, ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 na wengine 250 kuchukuliwa mateka.
Israel inasema imeshawauwa wanamgambo 13,000 hadi sasa, ingawa haijatowa ushahidi wowote.