Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu Dk Manguruwe.
Dk Manguruwe na mwenzake Rweyemamu John (59) ambaye ni mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiweno ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Rweyemamu yupo nje kwa dhamana kwa sababu hana mashtaka ya kutakatisha.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na kuangaliwa iwapo upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Kasala ametoa taarifa hiyo, mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.
“Leo kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa wa kwanza (Mkondya) hajaletwa mahakamani hapa na tumejaribu kuahirisha kesi hii kwa njia ya video lakini mawasiliano hayakuwa mazuri, lakini mshtakiwa wa pili yupo mbele ya mahakamani hapa,” amesema wakili Kasala.
Kasala amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kwamba upande wa mashtaka unaomba tarehe nyingine ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi umekamilika.
Hakimu Magutu ameahirisha hadi Januari 29, 2025 itakapotajwa na mshtakiwa Mkondya yupo rumande wakati John yupo nje kwa dhamana.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28, mashtaka 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha viwanja.
Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi 2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo
Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuijipatia kiasi cha Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika mashtaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.
Inadaiwa kuwa Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya Uhujumu Uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.