Musoma. Baadhi ya wadau wa sekta ya kodi mkoani Mara wamependekeza kupunguzwa kwa wingi wa kodi ili kuimarisha uchumi wa taifa. Wamesema hatua hiyo itahamasisha ulipaji wa hiari wa kodi na kuchangia ongezeko la pato la Taifa.
Wadau hao wamesisitiza umuhimu wa kuunganisha baadhi ya kodi na tozo ili zikusanywe na taasisi moja badala ya mfumo wa sasa wa taasisi nyingi zinazokusanya kodi na tozo zaidi ya mbili kwa biashara moja. Wakizungumza leo Jumatano Januari 15, 2025 katika kikao cha Tume ya Rais ya Maboresho ya mjini Musoma, wadau hao wamesema wingi wa kodi unaongeza gharama za uendeshaji wa biashara, hali inayosababisha biashara nyingi kufungwa.
Meshack Kajira, mfanyabiashara wa madini amesema sekta ya madini ni miongoni mwa inayoteswa na utitiri wa kodi.
Amesema wanatoza kodi ya asilimia 6 na Tume ya Madini, asilimia moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na asilimia 0.3 inatozwa na halmashauri.
Hivyo, amependekeza kodi hizo zipunguzwe na kubaki ile ya asilimia sita inayotozwa na taasisi moja ili kurahisisha mazingira ya biashara.
“Ninapendekeza kuwepo kodi ya asilimia sita kwenye biashara hii na itozwe na taasisi moja huku serikali ikiweka mifumo yake vizuri kuangalia namna gani taasisi zake zitapata mgawo wa hiyo asilimia 6 kwa maana kuwa mifumo ya serikali isomane,” amesema Kajira.
Naye mfanyabiashara wa vifaa vya shule, Gerson Kayola amependekeza kuwepo kwa taasisi moja ya ukusanyaji wa kodi na mfumo wa leseni moja kwa biashara moja ili kupunguza gharama zisizo za lazima.
“Dukani kwangu nina leseni zaidi ya tatu ambazo nimekata kwa mamlaka tofauti na zote nazilipia sasa unajiuliza biashara moja inakuwa na leseni zote hizo kwaajili ya nini, kwanini kusiwe na mfumo maalum wa kukata leseni moja kwaajili ya biashara moja hii itatupunguzia gharama zisizokuwa za lazima,” amesema Kayola.
Amina Omari alilalamikia utitiri wa kodi zinazotozwa na halmashauri, zikiwamo leseni, ushuru wa huduma, usafi na zimamoto, akisisitiza kuwa kodi hizo zinabebesha mzigo mkubwa wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea huduma hizo.
“Naomba hizi kodi zipunguzwe mfano huu ushuru wa huduma hivi kazi yake ni nini wakati pamoja na kuulipa bado natakiwa nilipie usafi manispaa, nikitumia choo natakiwa kulipa nikitaka hufuma ya zima moto natakiwa nilipie wakati huo TRA nalipa mapato sasa hii huduma tunayolipia ni ipi,” amehoji.
Mfanyabiashara wa madini, Hezbon Joseph kwa upande wake amelalamikia makato ya kodi kuwa mengi hali inayowafanya wafanyabiashara kuhofia kuweka fedha zao benki kwa sababu ya kutozwa kodi mara mbili.
Awali, Balozi Maimuna Tarishi, mjumbe wa Tume hiyo, aliwasihi wadau kushiriki kikamilifu kutoa maoni yao kupitia vikao, simu, barua pepe na dodoso linalopatikana mtandaoni, ili kusaidia kutatua changamoto za kodi nchini.
“Ili kuweza kupata utatuzi wa kudumu kwa changamoto hizi ni vema watanzania wote tukashiriki kutia maoni yetu kupitia vikao kama hivi, simu, parua pepe pamoja na kujaza dodoso linalopatikana kwenye mitandao ya tume pamoja na kwenye tovuti ya tume,”amesema Balozi Tarishi.