Michelle Obama adaiwa kususia uapisho wa Trump

Washington. Zikiwa zimebaki siku tano kuapishwa kwa Rais Mteule wa Marekani Donald Trump, Michelle Obama ambaye ni mke wa Rais mstaafu wa Marekani, Baraka Obama amesema hatashiriki hafla ya kumuapisha Rais huyo.

Trump anatarajiwa kuapishwa jijini Washington DC, Januari 20, 2025, hafla ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na wanasiasa, watu mashuhuri na viongozi wa nchi na wanadiplomasia kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.

CNN imeripoti kuwa taarifa ya Michelle kutoshiriki uapisho huo imethibitishwa na ofisi yake leo Jumatano Januari 15, 2025, bila kueleza sababu ya mwanamke huyo maarufu kama nchini humo.

“Rais Mstaafu Baraka Obama amethibitisha kushiriki uapisho wa Rais Donald Trump. Hata hivyo mke wake, Michelle Obama hatahudhuria hafla hiyo,” imesema taarifa hiyo ya Ofisi ya Barack na Michelle Obama.

Uamuzi wa kutoshiriki uapisho huo umeibua maswali kutokana na utamaduni uliojengeka nchini humo kuonyesha kuwa marais wastaafu na wake zao hutakiwa kushiriki hafla za uapisho wa marais wateule nchini humo.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu George Bush, amethibitisha kushiriki hafla hiyo na ofisi yake imethibitisha kushiriki hafla hiyo sambamba na Rais mstaafu, Bill Clinton na mkewe, Hillary Clinton.

Michelle Obama pia hakuonekana wakati wa ibada ya kuaga mwili wala maziko ya aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Jimmy Carter badala yake aliendelea kubaki eneo la makazi yao yaliyopo Hawaii nchini humo.

Katika hafla hiyo, Rais Barack Obama alihudhuria katika ukumbi wa kitaifa ilipofanyika ibada ya kuaga mwili wa Carter ambaye anatajwa kuwa Rais aliyependwa na Marekani na ulimwengu kutokana na aina yake ya maisha ya kutopenda kujilimbikizia mali.

Katika hafla ya kuaga mwili wa Carter, Obama alionekana akiwa amekaa pembeni ya Rais mteule, Trump huku wakizungumza.

Wenza wa viongozi wa taifa hilo ambalo pia walishiriki hafla ya kumuaga Carter ni pamoja na Hillary Clinton na Laura Bush.

Michelle Obama amekuwa akitamka wazi kuhusiana na kutopendezwa na mwenendo na tabia ya Trump, huku akisema Rais huyo amekuwa akiiweka familia yake mashakani kutokana na kauli zake majukwaani.

Mwaka 2017, alitajwa kuweka hisia hizo pembeni baada ya Trump kushinda uchaguzi mkuu nchini humo, ambapo miongoni mwa mambo aliyoyafanya Michelle ni pamoja na kumkaribisha Mke wa Trump, Mellania katika Ikulu ya Taifa hilo kabla ya kukabidhi madaraka.

Miaka kadhaa baadayee, Michelle alifunguka mwaka 2023 kuhusiana na uzoefu wake alipokuwa jukwaani akishuhudia uapisho wa Trump kuwa Rais wa taifa hilo mwaka 2017.

Kama ilivyo kwa Michelle, Trump na mkewe, Mellania hawakushiriki katika hafla ya kumuapisha Rais Joe Biden kuwa Rais wa taifa hilo mwaka 2020, wakilalamikia uchaguzi huo.

Musk, Bezos na Zuckerberg kushiriki

Mbali na wanasiasa hao, mabilionea wa taifa hilo nao wamethibitisha kushiriki katika uapisho wa Rais Trump siku ya Jumatatu ijayo.

Miongoni mwa mabilionea waliothibitisha kushiriki ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Tesla, ambaye amekuwa mtu wa karibu wa Trump siku za hivi karibuni.

Pia, kutakuwa na ushiriki wa bilionea, Jeff Bezos, ambaye ni mwanzilishi wa Mtandao wa Amazon na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Meta, Mark Zuckerberg, inayomiliki mitandao Facebook na WhatsApp.

Wakati hao wanatajwa kuwa wataketi karibu na atakapokuwa amekaa Trump na baraza lake, kwa mujibu wa maofisa na kamati ya maandalizi ya shughuli hiyo.

Jeff Bezos na Zuckerberg walikutana na Trump katika makazi yake yaliyopo eneo la Mar-a-Lago mwezi Novemba muda mfupi baada ya Trump kutangazwa kushinda uchaguzi huo dhidi ya mshindani wake, Kamala Harris wa Chama cha Democrats anachotokea Rais Joe Biden.

Zuckerberg ni miongoni mwa mabilionea ambao walikubali na kujitolea kuchangia kiasi cha Dola za Marekani 1 milioni (Sh2.5 trilioni).

Facebook pia ambayo inamilikiwa na Zuckerberg mwezi uliopita ilitoa taarifa kwa umma kuwa itatumika ipasavyo kutekeleza Sera ya Teknolojia inayosukumwa na uongozi wa Trump.

Amazon nayo ilichangia Dola bilioni 1 katika sherehe za uapisho wa Rais Trump kama alivyofanya, Mark Zuckerberg.

Katika hali ya kushangaza, Makamu wa Rais Mteule, JD Vance na familia yake hawajapewa mwaliko wa kutembelea Ikulu ya Taifa hilo kwa ajili ya kukabidhiwa majukumu na mtangulizi wao katika nafasi hiyo, Kamala Harris.

Kwa mujibu wa CNN, maofisa wawili wa Ikulu ya taifa hilo, wamethibitisha kuwa Harris amegoma kutoa mwaliko kwa JD Vance na familia yake kama ulivyo utamaduni wa taifa hilo kwa watangulizi kuwaalika viongozi wapya kwa lengo la kuwakabidhi Ofisi.

Harris na Vance hawajawahi kuzungumza kati Novemba 2024, wakati wa uchaguzi uliofanyika nchini humo, Mshauri wa Vance aliieleza CNN. Kitendo cha Kamala Harris kushindwa uchunguzi huo kinatajwa kuwa chanzo cha mgomo huo wa Harris.

Wakati zikibakia tano kuapishwa kwa Trump, Rais Joe Biden anatarajiwa kutoa hotuba yake ya mwisho kwa raia wa taifa hilo, yenye lengo la kuwaaga na kwenda kupumzika katika wadhfa huo.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa Biden kutoa hotuba hiyo katika Ofisi yake ya Oval nchini humo alipotangaza uamuzi wake wa kujitoa kugombea katika kinyang’anyiro cha nafasi ya urais wa taifa hilo Julai 2024.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts