Doha. Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Jeshi la Israel (IDF) na kundi la wapiganaji la Hamas lililopo ukanda wa Gaza nchini Palestina yamefikia pazuri.
Kwa mujibu wa tovuti ya Al Jazeera, masungumzo ya makubaliano ya kusitisha mapigano hayo yanayoratibiwa na mataifa mbalimbali ikiwemo Qatar na Marekani yanaendelea vyema jijini Doha Qatar.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed al-Ansari, pande zote za mzozo huo zimekaribia kukubaliana na masharti ya kila upande kuhusiana na hatua ya kusitisha vita hiyo.
Ansari ametoa taarifa hiyo leo jana Jumanne Januari 14, 2025, alipozungumza na kutoa mrejesho wa mazungumzo hayo kwa vyombo vya Habari nchini humo.
Waratibu wa mazungumzo hayo ya amani ni Qatar, Marekani ha Misri ambao wamekuwa wakipambania kusitishwa kwa vita hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miezi 13.
“Andiko la kwanza la makubaliano hayo limekabidhiwa kwenye pande zote Hamas na Israel na vikwazo vikubwa vilivyokuwa vinakwamisha kufikia makubaliano hayo vimeshatatuliwa.
“Mazungumzo yanayoendelea sasa hivi yanalenga kuweka sawa masuala madogo madogo tu yaliyokuwa yamebaki. Ninaweza kuweka wazi kuwa leo (jana) tumekaribia kufikia hatma ya kusitisha vita hiyo,” amesema al-Ansari.
Ametabiri kuwa huenda vita hiyo ikakoma mara tu baada ya kukamilisha kwa nyaraka za makubaliano ya pande zote toleo la Mwisho.
“Tunaamini kwamba sisi (Qatar) tunaweza, kupitia mazungumzo ya pande zote na washirika wetu Misri na Marekani, tutaondoa tofauti zilizopo kati ya pande zote za mzozo huu,” ameongeza al-Ansari.
Wakati huo, al-Ansari ameonya jamii na maeneo mbalimbali ulimwenguni kuondoa matumaini makubwa kuhusiana na kusitishwa kwa mapigano hayo hadi pale taarifa rasmi itakapotolewa.
“Tunaamini kwamba tuko katika hatua nzuri ya kumaliza mzozo huu, na tunaamini kuwa tuko katika hatua ya mwisho kabisa ya mazungumzo lakini ili kujiridhisha na kujipa uhakika ni hadi pale taarifa rasmi itakapotangazwa ya kusitishwa mapigano.
“Hivyo basi hatupaswi kuanza kushangilia sana mapema hivi, juu ya kinachoendelea japo tunapaswa kuwa na matumaini kwamba tulipofika ni pazuri,” alisema.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitarajiwa kuitisha kikao nyeti cha viongozi wa Juu wa Ulinzi katika taifa hilo, jana Jumanne kuzungumzia mazungumzo hayo yenye lengo la kusitishwa kwa vita hiyo.
Mwandishi wa Al Jazeera, Hamdah Salhut akiripoti kutokea Jordan alisema taarifa za Netanyahu kuitisha kikao hicho ni za uhakika huku akisema bado haijawekwa wazi kuwa kikao hicho kiliazimia kitu gani.
“Kumbuka Netanyahu kwa zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akinukuliwa akisema kuwa hata kama hakutakuwa na kusitishwa kwa mapigano, lengo la IDF litabakia pale pale ambalo ni kuwarejesha mateka wake na kuyamaliza makundi anayoyaita ni ya kigaidi yaliyopo eneo la Gaza,” amesema.
Marekani, Misri na Qatar zimetumia mwaka mzima wa 2024, kupambana kuhakikisha kwamba vita hiyo inakomeshwa na kufanikisha kuachiwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa eneo la Gaza tangu shambulio la Oktoba 7, 2023.
Inaelezwa kwamba takriban raia 100 wa Israel wanaendelea kushikiliwa mateka na wapiganaji wa Hamas eneo la Gaza huku angalau robo ya mateka hayo wakihofiwa kuwa tayari wameuawa.
Maelfu ya raia wa Israel pia wamedaiwa kuuawa wakati wa uvamizi wa Hamas nchini Israel siku hiyo (Oktoba 7, 2023).
Kwa mujibu wa taarifa zilizovuja kwenye vyombo vya habari nchini Israel, zinadai kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano hayo yamegawanywa katika hatua tatu tofauti.
Katika hatua ya kwanza, mateka 33 wa Israel kati ya 100 wanaoshikiliwa eneo la Gaza wataachiwa na Israel itawaachia raia 50 wa Palestina wanaoshikiliwa kama wafungwa katika magereza nchini Israel kwa kila mwanajeshi wa Israel anayeshukiliwa eneo hilo.
Pia waPalestina 30 wataachiwa kwa kuzingatia mateka wanaoshikiliwa eneo la Gaza kama mateka.
Awamu ya pili ya makubaliano hayo, inadaiwa kuwa itaanza kutekelezwa baada ya siku 16, ambapo utajikita katika hatua ya kuachiliwa kwa wafungwa waliosalia huku hatua ya tatu na ya mwisho inahusisha kuweka makubaliano ya muda mrefu yenye lengo la kuanzisha uongozi mpya wa Gaza na kulijenga upya eneo la ukanda wa Gaza.
Ripoti hizo zinadai kuwa makubaliano hayo, yanaitaka Israel kuondoa kabisa vikosi vyake vya kijeshi eneo la Gaza hususan ni eneo la Korido ya Philadelphia ambalo ni eneo linalotenganisha Taifa ya Misri na Gaza.
Kundi la Islamic Jihad lenye makao yake eneo la Gaza pia linadaiwa kupeleka wawakilishi Jijini Doha Qatar kwa ajili ya kushiriki hatua ya mwisho ya makubaliano hayo ili kusitisha mapigano kati ya pande hizo.
Tangu kuanza Operesheni zake eneo la Gaza Oktoba 7, 2023, Jeshi la Israel linadaiwa kuwasababisha vifo vya raia 46,645 wa Palestina na kujeruhi 110,012 huku raia 1,139 wa Israel wakidaiwa kuuawa kwenye vita hiyo na zaidi ya 200 wakichukuliwa mateka.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.