Miili saba kati ya 11 ajali ya Handeni kuzikwa, majonzi yatawala

Handeni. Miili ya watu 11 waliopoteza maisha katika ajali ya lori katika Kijiji cha Chang’ombe, Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni, imetambuliwa na baadhi imeshazikwa na mingine utaratibu unaendelea.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Januari 13, 2025, baada ya lori kuwagonga watu waliokuwa wakitoa msaada kwa majeruhi wa ajali nyingine ya gari aina ya Tata.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji Korogwe, Miriam Cheche ameiambia Mwananchi Digital leo Jumatano, Januari 15, 2025, kati ya majeruhi 13 waliopokewa hospitalini hapo, watano bado wapo chini ya uangalizi, huku wawili wakisafirishwa jana kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga (Bombo) kwa matibabu zaidi.

Baadhi ndugu wakiwa chumba cha kuhifadhia Maiti hospitali ya Halmashauri ya Mji Korogwe Magunga kwaajili kuchukua miili ya ndugu zao kwa shughuli za mazishi.Picha na Rajabu Athumani

Dk Cheche amesema majeruhi wawili wamepelekwa Bombo kutokana na majeraha makubwa.

Amesema mmoja amekatika mguu na mwingine ana majeraha makubwa kichwani.

“Majeruhi waliobaki watano wanaendelea kupata nafuu na wanaweza kuruhusiwa muda wowote,” amesema.

Kuhusu miili ya marehemu, Dk Cheche amesema yote imetambuliwa baada ya ndugu kufika hospitalini hapo jana.

Amesema na ilikabidhiwa kwa familia zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Akizungumzia ajali hiyo leo, Diwani wa Segera, Onesmo Makomelo amesema miili saba tayari imezikwa na minne bado haijazikwa.

Amesema marehemu saba wamezikwa katika vijiji vya Mailikumi, Chang’ombe na Kwamgwe vilivyopo katika Kata ya Segera na mmoja umesafirishwa kuelekea Bukoba mkoani Kagera na mwili mmoja unaenda kuzikwa Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Wengi wa waliofariki ni vijana waliokuwa wakijishughulisha na biashara ndogondogo kama kuuza machungwa barabarani. Tukio hili limeacha majonzi kijijini,” amesema Diwani Makomelo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema Serikali inagharamia shughuli zote za mazishi, usafirishaji wa miili na matibabu kwa majeruhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema juhudi za kumsaka dereva wa lori lililowagonga watu hao, Baraka Merkizedek, zinaendelea.

Dereva huyo anatuhumiwa kusababisha ajali hiyo iliyoua watu 11 na kujeruhi 13 na Kamanda Mchunguzi ameomba wananchi kutoa taarifa itakayosaidia kukamatwa kwake.

Ajali hiyo ilitokea wakati watu walipokuwa wakitoa msaada kwa majeruhi wa ajali ya gari aina ya Tata, iliyotokea kijijini hapo. Katika ajali ya awali, hakuna vifo vilivyotokea, bali majeraha madogo.

Related Posts