Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimepuliza kipenga kwa wanachama wake wenye sifa za kugombea uongozi katika Uchaguzi Mkuu 2025 kuanza kutangaza nia.
Nafasi wanazotakiwa kujitokeza kuwania katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu ni za udiwani, udiwani viti maalumu, ubunge, ubunge viti maalumu na urais.
ACT-Wazalendo kinakuwa chama cha kwanza kati ya vyama 19 vya siasa vilivyopo nchini kuwaruhusu wanachama wake kutia nia na kujitangaza kugombea uongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Januari 15, 2025, jijini Dar es Salaam amesema: “ACT-Wazalendo kinawatangazia Watanzania mchakato wa kutangaza nia za kugombea urais, ubunge na udiwani umefunguliwa leo Januari 15, 2025. Tamko hili ni utekelezaji wa azimio la Halmashauri Kuu ya ACT-Wazalendo iliyoagiza chama kiweke utaratibu na kuratibu utangazaji wa nia wa nafasi hizo.”
Amesema kila mwanachama mwenye sifa ya kugombea anatakiwa kujisajili. Ado amesema wanaowania udiwani watajisajili ngazi ya kata, ubunge ngazi ya jimbo na urais ofisi ya katibu mkuu.
Amesema watia nia wanaweza kujitangaza kwa njia mbalimbali kupitia vyombo vya habari, akisisitiza kuwa michakato yote ya watia nia itaratibiwa na chama hicho.
Viongozi wa kata na majimbo wameagizwa kuwaruhusu watia nia kutumia ofisi za kata, majimbo na mikoa kutangaza nia. Kwa nafasi ya urais, ofisi ya makao makuu ya chama ndiyo itatumika.
Amewataka watia nia kujipima iwapo wana sifa za kugombea kulingana na Katiba ya ACT-Wazalendo na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sifa nyingine amesema ni uwezo wa kujieleza na haiba ya nafasi anayotarajia kugombea.
“Kabla ya kuomba nafasi ya kugombea urais, jiulize kama una sifa za kuongoza Tanzania, una maono ya kuongoza na maadili ya kuongoza Tanzania,” amesema.
Ado amesema kila mtia nia atapimwa kwa namna anavyoshiriki ujenzi wa chama, akisisitiza kila mmoja ana nafasi katika ujenzi wa chama.
Amewaagiza viongozi wa chama hicho ngazi za chini kutunza rekodi za ushiriki wa wanachama katika ujenzi wa chama hicho, akieleza kuwa taarifa hizo zitatumika kama rejea kwa wagombea namna walivyokijenga chama.
Ado amesema tangazo la kuitisha wenye sifa za kugombea ni maandalizi ya uchaguzi japokuwa wana madai, hawapaswi kushinikiza bila kujiandaa na uchaguzi.
Chama hicho kimekuwa kikishinikiza kupatikana kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kikidai iliyopo siyo huru.
“Kilichobadilika ni jina lakini masuala mengi ya msingi hayakuzingatiwa. ACT-Wazalendo tumesema tutashirikiana na wadau wengine wa demokrasia kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unasimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi. Hata uchaguzi wa serikali za mitaa ulipokwisha tulisema hatuutambui,” amesema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Paul Loisulie, amesema hatua ya ACT-Wazalendo kutoa ruksa kwa wanachama wake kutangaza nia mapema ni fursa ya chama kujitangaza.
Amesema tofauti na Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachowaza namna ya kupunguza watu kipindi cha uchaguzi, ACT-Wazalendo kina uchache wa rasilimali watu hivyo kuanza mchakato mapema ni jambo zuri.
“Jambo la tatu, naiona ACT-Wazalendo imefanya hivi kujenga uwazi. Unapoanza namna hii kuruhusu watu kujitokeza, unataka kujenga uwazi ndani ya chama,” amesema.