Nchi sita muhimu kwa uchumi wa Tanzania

Miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa nchi ni ufanisi wa biashara wa ndani na nje unaohakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu nchini, lakini pia chanzo cha mapato ya kigeni kupitia mauzo ya nje ya nchi.

Serikali na sekta binafsi katika nchi yoyote hufanya juhudi za kuhakikisha inakuza mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kwa ajili ya kupata uhakika wa bidhaa zinazohitajika, lakini pia masoko ya bidhaa zinazozalishwa ndani.

Kwa Tanzania katika kipindi cha miaka mitano mfululizo, imekuwa ikitegemea zaidi bidhaa kutoka nchi 6 duniani ili kukidhi mahitaji yake, ripoti ya mwaka ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) 2023/2024 inaeleza.

Ripoti hii inazitaja nchi za China, India, Japan, Saudi Arabia, Afrika Kusini na Falme za Kiarabu (UAE) kama chanzo kikubwa cha bidhaa za Tanzania zitokazo nje na kiwango kutoka katika kila nchi kimekuwa kikiongezeka.

Ripoti hii ambayo inaangazia vitu mbalimbali, inaitaja China kama nchi yenye mauzo makubwa zaidi Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo. Mwaka 2023/2024 pekee Sh10.9 trilioni zimetumika kununua bidhaa mbalimbali kutoka nchi hiyo, kiwango ambacho ni mara mbili zaidi ya kilichotumika mwaka 2019/20 kilichokuwa Sh4.56 trilioni.

China, ilifuatiwa kwa karibu na nchi ya India ambayo katika mwaka 2019/20 jumla ya Sh3.02 trilioni zilitumiwa na Tanzania katika kununua bidhaa mbalimbali, fedha ambayo imeongezeka hadi kufikia Sh5.56 trilioni mwaka 2023/2024.

Falme za Kiarabu mwaka 2019/20 iliiuzia Tanzania bidhaa za Sh2.072 trilioni, kiwango ambacho nacho kimeongezeka zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi cha miaka mitano hadi kudikia Sh4.005 trilioni mwaka 2023/2024.

Japan nayo ni miongoni mwa nchi ambazo zilishuhudia ukuaji wa soko la bidhaa zake katika ardhi ya Tanzania, kwani mwaka 2019/20 ilifanya biashara ya Sh906.15 bilioni pekee, kiwango ambacho kilikua hadi kufikia Sh1.475 trilioni mwaka 2023/2024.

Nchi ya Afrika Kusini nayo iliibuka huku bidhaa zake zikigharimu Sh1.409 trilioni za Watanzania katika mwaka 2023/2024, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh977.68 bilioni mwaka 2019/20.

Kwa upande wa Saudi Arabia mwaka 2019/20 ilifanya mauzo ya bidhaa nchini Tanzania yenye thamani ya Sh613.852 bilioni ambayo iliongezeka hadi Sh1.388 trilioni.

Kuhusu utegemezi, mchambuzi wa uchumi, Dk Donald Mmari anasema kama nchi ili iweze kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nchi hizo ni vyema kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuweza kuzalisha bidhaa zitakazofaa katika matumizi ya ndani na ziwekwe katika kiwango cha kuweza kushindana katika masoko ya nje.

Anasema hilo litawezekana kwa kuweka nguvu katika uwekezaji wa teknolojia kwa sababu nchi ambazo Tanzania inanunua bidhaa sana ziko mbele kiteknolojia.

“Ili kujua wapi tunapaswa kuwekeza ili tuuze zaidi, tunaweza kutumia tafiti ambazo zimewahi kufanywa kwani zipo na zinaonyesha wapi tukiwekeza tunaweza kupata hela zaidi. Eneo kama madini tunazalisha na kuuza kwa wingi, tuongeze thamani na tuuze bidhaa zake kwa bei ghali badala ya kuwauzia kama malighafi wakazalishe warudishe nchini watauza kwa bei kubwa,” anasema Dk Mmari.

Mbali na madini, anasema ngozi ni eneo jingine linaloweza kutumika ipasavyo katika kuleta fedha za kigeni kwa kuzalisha bidhaa zinazoweza kupatikana ndani yake na kuziuza katika masoko mbalimbali.

“Tuna mifugo mingi lakini ngozi zinachukuliwa na kwenda kutengeneza nje, tuwekeze katika teknolojia kwa kuweka mazingira safi ya uwekezaji yatakayochochea uzalishaji wa bidhaa kwa wingi, kwa gharama nafuu ili ziweze kuuzwa kwa bei shindani,” anasema DK Mmari.

Wakati Tanzania ikitumia mabilioni ya Dola kununua bidhaa katika nchi hizo, upande mwingine wa Shilingi unaonyesha kuwa kati ya mataifa hayo sita, matano ni wanunuzi vinara wa bidhaa za Tanzania kwa.

Kwa mwaka 2023/2024, China ilinunua bidhaa za Tanzania za Sh1.115 trilioni, India ikanunua bidhaa za Sh4.08 trilioni, Afrika Kusini bidhaa za Sh4.016 trilioni, Nchi za Jumuiya za Kiarabu zikinunua bidhaa za Sh1.467 trilioni.

Japan ndiyo nchi pekee katika orodha ya nchi sita ambazo Tanzania ilinunua zaidi kutoka kwao ambayo iliagiza bidhaa za Tanzania kwa kiwango kidogo, kwani ilitumia Sh178.95 bilioni pekee.

Tofauti na kutegemea nchi zilezile katika kufanya nazo biashara, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano anasema kupanuka kwa soko lolote huwa ni vizuri si tu idadi ya wanunuzi iongezeke, bali pia kiasi cha bidhaa wanachonunua pia kuongezeka.

“Idadi ya nchi wanunuzi kubaki palepale si afya sana, ila si mbaya kama wananunua bidhaa nyingi kama takwimu zilivyo na kununua kwa thamani kubwa zaidi kuliko ilivyo awali,” anasema Lutengano na kuongeza:

“Bado tuna fursa nzuri ya kupanua soko ili mauzo yaendelee kuongezeka na kuleta motisha zaidi kwa wazalishaji nchini na kuendelea kukuza uchumi,” anasema.

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dk Felix Nandonde anasema kilichoonekana huenda kinatokana na jitihada zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika uboreshaji wa mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbalimbali ambayo ilifanya mikataba mbalimbali ya mashirikiano kusainiwa, ikiwemo ya biashara.

Jambo hilo liliongeza kasi ya ufanyaji wa biashara kati ya nchi hizo, akitolea mfano wa India na China ambapo bidhaa kutoka Tanzania zilipata masoko ya uhakika katika nchi hizo, wakati wao pia wakiuza bidhaa zao nchini.

“Kama nchi ni lazima tupanue soko kubwa la walaji wetu wa ndani, kutanua matumizi ya teknolojia ya kuongeza thamani ya mazao hayo na kuvutia viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao yanayozalishwa,” anasema.

Jambo hilo litasaidia kama nchi kuongeza thamani ya mazao inayozalisha badala ya kuyauza nje kama malighafi ambayo itakwenda kutengeneza vitu mbalimbali na kurudishwa tena nchini kuuzwa kwa bei ghali.

“Katika mikakati iliyopo ni vyema kuangalia wapi tulifanikiwa, jitihada zipo na zinafanyika katika kupiga debe uongezaji wa thamani lakini tuongeze nguvu zaidi tuache kuuza bidhaa ghafi,” anasema Dk Nandonde.

Mtaalamu wa Biashara, Oscar Mkude anasema nchi inanunua kutoka nje bidhaa na huduma ambapo ndani yake kuna mashine ambazo zinatumika katika uzalishaji, bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa ambazo ndani ya nchi hazipatikani.

“Mara nyingi sisi tunapeleka kahawa tena ghafi, ni wachache wanaofanya uongezaji thamani, hata chai nyingi inakwenda ghafi, kama imeongezwa thamani ni kidogo sana, kitu kama dhahabu vilevile inauzwa ikiwa ghafi au imechenjuliwa kidogo,” anasema Mkude.

Anasema kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa nje ndiyo jibu sahihi, lakini utekelezaji wake unahitaji watu kujipanga, kwani ili uongeze thamani mfano dhahabu ni lazima uwe na uwezo wa kufanya jambo hilo.

“Kwenye madini hili limeshaanza, nafikiri hili litakuwa linafanyika wakati ambao uwezo wa kitaalamu umeshajengwa kwa watu ili waweze kufanya kazi hii, hili linatakiwa pia kufanyika katika bidhaa nyingine, hii itasaidia sana kupunguza urari wetu wa biashara,” anasema Mkude.

Anasema ni vyema kuunganisha mnyororo wa sekta ya uzalishaji na sekta ya viwanda kwa kuwahamasisha watanzania kuzalisha kwa wingi ili kuweza kuvilisha viwanda vitakavyoanzishwa Tanzania.

“Ni ngumu kufungamanisha sekta ya kilimo na uzalishaji, kwa sababu kilimo tunachokifanya bado hakitoshi kuhudumia viwanda vyetu, inabidi nguvu iongezeke, tija katika kilimo iongezeke ili kuweza kupata matokeo tunayoyatarajia,” anasema Mkude.

Related Posts