Teknolojia ya kidijitali ilikuwa miongoni mwa mada kuu katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2023, COP29, ambapo viongozi wa dunia walijadili athari za ukuaji wa sekta ya teknolojia.
Kwa mara ya kwanza, mkutano huo wa kimataifa ulikuwa na siku maalumu ya kidijitali (Digitalization Day) ambapo walitoa ahadi za kuhamasisha matumizi ya suluhisho za kidijitali na kupunguza matumizi ya rasilimali za teknolojia.
Katika mkutano hao wadau wa teknolojia waliazimia na kuungwa mkono katika mpango wao wa kushiriki mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Itakumbukwa kuwa toleo la mwaka 2019 la Ripoti ya Athari ya Sekta ya Simu kwa Maendeleo Endelevu ya GSMA lilionyesha mchango ulioongezeka wa sekta ya simu katika kufanikisha Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa na kutoa wito kwa watoa huduma kuongeza juhudi kabla ya mwaka 2030.
Baada ya mkutano huo mabadiliko yalishuhudiwa katika kampuni tofauti, wapo walioanza kutengeneza mipango mikakati ya kusaidia mabadiliko ya tabianchi na wengine kuweka kipengele cha mazingira katika ripoti zao ili kusisitiza ufuatiliaji.
Karibu kampuni zote zimeweka mikakati ya utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha zinachangia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kupitia shughuli na huduma wanazotoa.
Mathalani, katika ripoti ya Vodacom Tanzania inayoeleza utekelezaji wa kampuni hiyo katika eneo la mazingira na uendelevu, walieleza namna ambavyo ubunifu na hatua za makusudi wanazochukua zinavyosaidia kulinda mazingira.
“Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa kwa shughuli zetu, minyororo ya thamani, na nchi tunazofanyia kazi. Tunakabiliana na tatizo hili kwa juhudi zetu za kupunguza athari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi na hatari zinazoweza kujitokeza,” ilieleza ripoti ya ESG ya kampuni ya Vodacom Tanzania, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu Philip Besiimire.
Katika ripoti hivyo Vodacom inaeleza kuwa itaendelea kupunguza matumizi ya plastiki kwa kuweka mbadala wake katika maeneo mengi ya huduma zao.
“Pale plastiki inapohitajika, tunatumia plastiki zilizorejelewa. Tangu 2017, kadi za SIM za aina ya “trio” zimeokoa tani 210.8 za plastiki, huku tani 30.8 zikiwa zimeokolewa mwaka 2024 pekee,” ilieleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana ilieleza kuwa huduma za e-SIM zilizozinduliwa mwaka 2015 zimevutia watumiaji zaidi y15,000. Mfumo huo wa kadi pia umepunguza hitaji la kubadilisha SIM kwa wateja wanaobadilisha vifaa.
Kampuni hiyo inasema wamekuwa na programu za usimamizi wa taka zinazohusisha kuhakiki matumizi yao, kufanya maamuzi endelevu, na kushirikiana na wasambazaji kupunguza taka za mazingira.
Kwa mfano, huduma za malipo ya kidijitali kupitia M-Pesa na programu zimechangia kupunguza takriban tani 214.4 za taka za karatasi mwaka wa fedha 2023, na kupunguza zaidi ya tani 1,000 za taka za karatasi kwa miaka nane iliyopita.
Kadhalika Vodacom inasema inashirikiana na wadau wake kuharakisha kuunganishwa kwa mitambo yao kwenye gridi ya umeme, kupunguza matumizi ya jenereta za dizeli na kwa sasa, asilimia 89 ya minara yao imeunganishwa na gridi ya umeme, huku asilimia 6 ikiwa kwenye mseto wa nishati ya jua.
Ukiachilia mbali juhudi binafsi za Vodacom, kampuni za simu nchini hivi sasa zinashiriki katika shughuli mbalimbali za kulinda mazingira, lakini pia zinatumia minara ya kuchangia, hali hiyo inapunguza ulazima wa kila mtandao wa simu kuwa mnara wake, hivyo kutumia nishati nyingi na kuchafua mazingira.
Kwa upande wa kampuni ya Airtel Africa, ambayo ni wamiliki wenza wa kampuni ya Airtel Tanzania, inasema katika maeneo inayotoa huduma imechukua hatua mbalimbali kupunguza athari za mazingira, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za kidijitali ambazo zinapunguza matumizi ya karatasi na ulazima wa watu kusafiri.
Ripoti ya uendelevu ya Airtel Afrika ya mwaka 2024 iliyosainiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu Olusegun Ogunsanya, ilieleza kuwa hatari kuu za mabadiliko ya tabianchi zinahusiana na ongezeko la mafuriko joto, na matukio ya hali ya hewa kali yanayoweza kuharibu miundombinu ya kimwili na kuathiri mapato.