Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu 27 wamefariki dunia baada ya machafuko ya siku moja tu.
Walioshuhudia wameripoti mashambulizi ya angani, makombora na makabiliano ya risasi yakirindima katika mji wa El-Fasher tangu Ijumaa iliyopita, ambapo taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema makabiliano yaliyodumu kwa saa nzima yalisababisha watu 850 kuachwa bila makao.
Umoja wa Mataifa pia unasema mawasiliano yamekatikakabisa katika mji huo huku wahudumu wa afya na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wakishindwa kutoa taarifa ya kinachoendelea kwa ulimwengu.
Hospitali ya watoto yashambuliwa
Mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba, vita hivyo vimeendelea hadi jana Jumapili ambapo mashambulizi ya makombora yamesababisha nyumba kuteketea.
Kulingana na shirika la misaada la Ufaransa la Madaktari Wasio na Mipaka MSF, shambulizi la angani lililofanywa na jeshi katika hospitali moja ya watoto, lilisababisha vifo vya watoto wawili na mhudumu katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Kote nchini Sudan zaidi ya asilimia 70 ya hospitali zimesitisha huduma zake tangu vita vianze jambo lililosababisha mzozo wa kiafya. Ripoti zinaarifu kuwa, wapiganaji wamekuwa wakiwalenga kimakusudi wahduumu wa afya, wameziteka hospitali na kuzigeuza kuwa kambi za kijeshi na zaidi ya hayo, wamekuwa wakipora na kuzuia vifaa vya matibabu kufika mahospitalini.
El-Fasher ndio mji wa mwisho mkuu huko darfur ambao hauko chini ya udhibiti wa wanamgambo wa RSF. Jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Marekani kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa wakitahadharisha kuhusiana na makabiliano kutokea katika eneo hilo.
Hayo yakiarifiwa, shirika moja la haki za binadamu lililo na makao yake nchini Uingereza limeripoti kuwa, mioto inayotumika kama silaha nchini Sudan, imesababisha uharibifu katika vijiji na miji magharibi mwa nchi hiyo tangu kuanza kwa vita nchini humo Aprili mwaka uliopita.
Moto kutumika kama silaha
Shirika hilo la Sudan Witness, limesema vijiji na makao 72 vimeharibiwa na moto mwezi uliopita na kupelekea jumla ya makaazi yaliyoharibiwa na moto nchini Sudan kufikia 201 tangua kuanza kwa vita.
Watafiti wa shirika hilo la Sudan Witness, wamechunguza mienendo ya moto kote katika nchi hiyo iliyozongwa na mapigano kwa kutumia mitandao wa kijamii, picha za setlaiti na data za kuchunguza moto.
Sudan imejikuta kwenye mapigano tangu Aprili mwaka jana kati ya jeshi linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.
Vyanzo: AFP/AP