Dar es Salaam. Baada ya Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) na Baraza la Wazee Chadema (Bazecha) kupata viongozi wake, leo ni zamu ya Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) kusaka viongozi katika sanduku la kura.
Uchaguzi huo wenye msisimko wa aina yake, unafanyika leo Alhamisi Januari 16, 2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam ambapo maandalizi ya mchakato huo tayari yamekamilika wajumbe, wagombea nao tayari wameanza kujongea katika ukumbi huo.
Kwa muda mrefu Bawacha imekuwa ikiongozwa na kaimu mwenyekiti, Sharifa Suleiman baada ya aliyekuwa Mwenyekiti Halima Mdee na Katibu wa baraza hilo, Grace Tendega na wenzao 17, kuvuliwa uanachama mwaka 2020.
Leo nafasi zinazowaniwa ni pamoja na Uenyekiti wa Bawacha, makamu mwenyekiti, wajumbe wa mkutano mkuu na wajumbe wa baraza kuu.
Huku nafasi za katibu na manaibu wake (Bara na Zanzibar) wakitarajiwa kupatikana kesho Ijumaa Januari 17, 2025 katika kikao cha kamati ya utendaji ya Bawacha.
Nafasi ya uenyekiti itazikutanisha sura tatu: Celestine Simba, Sharifa Suleiman na Susan Kiwanga.
Kwa upande wa makamu mwenyekiti upande wa Bara, sura zitakazochuana ni Agnes Chilulumo, Elizabeth Mwakikomo, Marietha Chenyenge, Moza Ally ,Naomi Ndigile, Rose Mkonyi na Salma Kasanzu na makamu mwenyekiti Zanzibar wagombea ni Bahati Haji na Zainab Bakari.