Dar es Salaam. Katika kuendana na soko la ajira linalohitaji rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa ikiwemo teknolojia, mradi mahususi wa kuwajengea uwezo wanafunzi wa vyuo vikuu umeanzishwa, ili kuwawezesha kushindana kwenye soko hilo.
Mradi huo uitwao (Generation Empower) ulioanzishwa na Taasisi ya Empower Limited una lengo la kuwawezesha vijana wa Tanzania kiujuzi ili kuziba pengo kati ya elimu ya kitaaluma na mahitaji ya soko, huku ikijenga nguvu kazi yenye ushindani na ubunifu.
Ujuzi unaotolewa kwa wanachuo kupitia mradi huo unahusisha kuandaa mapendekezo, kuzungumza mbele za watu, kujiamini pamoja na teknolojia ya mawasiliano (Tehama).
Akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa mradi huo ambapo Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kimesaini makubaliano na Empower Limited tayari kuanza utekelezaji Makamu Mkuu wa ARU, Profesa Evaristo Liwa amesema soko la sasa linataka watu wenye ujuzi kwa kuwa ushindani ni mkubwa.
“Mradi huu unaohusisha wanafunzi wa mwaka wa mwisho unasaidia kuongeza ujuzi kwa vijana wetu kwenda kushindana na soko la ajira. Sisi kama Chuo tunatazamia kuongeza ubora kwa wanafunzi wetu na ni fursa iliyokuja wakati sahihi,” amesema.
Amesema wanafunzi watapata ujuzi muhimu ili wajiandae kuwa viongozi, wasuluhishaji wazuri wa migogoro ya kwenye jamii hasa ya ardhi huku akisema hata kama akiajiriwa au kujiajiri basi lazima awe mtu mwenye kujiamini.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo taaluma utafiti na ushauri ARU, Profesa John Lupala amesema kwa sasa kuna mabadiliko makubwa ya kiteknolojia huku akitoa rai wanafunzi kufundishwa kuanzisha kampuni.
“Pia mbali na yote wanafunzi wanapaswa kufundishwa elimu ya fedha namna ya kuidhibiti ambayo ni muhimu si tu kwao bali kwa watu wote,” amesema Profesa Lupala.
Msimamizi wa mradi huo, Furahini Godlike amesema lengo la mradi linataka kubadilisha fikra za vijana kwa kujiamini waweze kuelewa soko la ajira linataka nini.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Empower Limited, Joshua Naiman amesema katika kipindi cha miezi sita mwanafunzi anajifunza ujuzi hadi pale atakapoingia katika soko la ajira.
Mwanafunzi wa Chuo cha Ardhi mwaka wa mwisho, Jemina Obeid amesema mradi utamaliza pengo la elimu ya taaluma wanayopata darasani na uhalisia wa soko la ajira ulivyo.