Mwakilishi maalumu wa EU ukanda wa  Maziwa Makuu azuru Tanzania

Dar es Salaam. Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya (EUSR) kwa Ukanda wa Maziwa Makuu, Johan Borgstam anaitembelea Tanzania kuanzia Januari 16 hadi 18, baada ya kufanya ziara  Burundi, DRC, Rwanda, Angola, Kenya, na Uganda, ikiwa ni juhudi zinazoendelea za ushirikiano wa kikanda.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya ofisi ya Tanzania leo Januari 16, 2025, imesema EUSR Borgstam anatarajia kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Waziri wa Ulinzi, Stergomena Tax na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Cosato Chumi, wanadiplomasia mashuhuri, wawakilishi wa sekta ya elimu ya juu na jamii ya kiraia nchini.

“Ziara hii inalenga kubadilishana mawazo kuhusu nafasi ya Tanzania katika ukanda wa Maziwa Makuu na kuthibitisha tena dhamira ya Umoja wa Ulaya katika kuendeleza amani, utulivu, na usalama katika ukanda huu kupitia Mkakati wa Umoja wa Ulaya wa Ukanda wa Maziwa Makuu,” imesema taarifa hiyo.

Akizungumzia ziara hiyo, Borgstam ameishukuru Tanzania kwa kushiriki moja kwa moja na wadau muhimu katika masuala ya kikanda.

“Tanzania ina jukumu muhimu katika kushughulikia mgogoro wa usalama na kibinadamu unaojitokeza katika sehemu za Ukanda wa Maziwa Makuu, ninathamini hali ya mazungumzo yetu kuwa chanya na yenye kujenga.

“Natarajia kuendelea kushirikiana kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania ili kukuza amani, utulivu, na usalama wa kikanda.”

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau amesisitiza uhusiano wa muda mrefu kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania.

“Umoja wa Ulaya unaendelea kuwa na dhamira ya kuunga mkono mazungumzo katika ukanda huu na kutoa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za kikanda kwa ajili ya Ukanda wa Maziwa Makuu.

“Ziara ya Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya kwa Ukanda wa Maziwa Makuu ni hatua nyingine muhimu katika dhamira yetu ya pamoja ya kushughulikia changamoto za sasa zinazoukabili ukanda huu,” amesema.

Borgstam aliteuliwa kuwa Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya (EUSR) mnamo Septemba 2024.

Dhamira yake ni kusaidia utekelezaji wa Mkakati Mpya wa Umoja wa Ulaya kwa Ukanda wa Maziwa Makuu, ambao malengo yake ni kuchangia amani, utulivu, na usalama kwa kupungua kwa mivutano, kuunga mkono mazungumzo na kutafuta suluhisho za muda mrefu kwa migogoro, hasa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Related Posts