Dodoma. Jeshi la Zima Moto na Uokoaji jijini hapa, limepewa mtambo wa kuzima moto wenye uwezo wa kufika kwenye jengo lenye urefu wa ghorofa 10 ikiwa ni sehemu ya mitambo 12 iliyokabidhiwa na Serikali kwa ajili ya shughuli za jeshi hilo.
Mikoa ya zimamoto na uokoaji iliyokabidhiwa mitambo hiyo ni pamoja na Dodoma, Ilala, Mwanza, Temeke, Kinondoni, Morogoro, Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.
Akikabidhi magari hayo leo Jumatatu Mei 13, 2024 na kuzindua nyumba za makazi ya askari wa jeshi hilo zilizopo Kikombo jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema mtambo huo wa kuzima moto kwenye majengo marefu ni wa pili nchini ambapo mwingine upo jijini Dar es salaam.
Masauni amesema kukabidhiwa kwa mitambo hiyo ya kuzima moto ni juhudi za Serikali katika kulipatia jeshi hilo vitendea kazi ili liweze kutekeleza majukumu ya kila siku.
Amesema mojawapo ya changamoto inayolikabili jeshi hilo ni uhaba wa vitendea kazi, lakini Serikali imeliona hilo na ndiyo maana limekabidhi magari hayo.
“Kumekuwepo na malalamiko ya wananchi kuhusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutofika kwa wakati pindi majanga ya moto yanapotokea, lakini wakati mwingine unakuta hilo lipo nje ya uwezo wao kutokana na ujenzi holela uliopo kwenye baadhi ya maeneo unaosababisha gari la kuzima moto lisifike kwa wakati kutokana na kukosekana kwa barabara,” amesema Masauni.
Amesema malalamiko mengine ni wananchi kudhani kuwa jeshi hilo linakwenda kwenye tukio bila ya kuwa na maji, jambo alilosema kuwa si kweli bali magari yaliyopo yana uwezo mdogo wa kubeba maji hivyo yanapokwisha ndani ya muda mfupi wanadhani kuwa walikwenda bila maji.
Amesema magari yaliyokabidhiwa leo yana uwezo wa kubeba maji lita 5,000 na fomu ya kuzima moto lita 500 hivyo uwezo wake kubeba lita 5,500, huku gari moja likiwa na uwezo wa kubeba maji lita 15,000.
Kuhusu vituo vya kujazia maji kutofanya kazi kutokana na kuwa vya muda mrefu, Waziri Masauni amesema kwenye bajeti ya mwaka huu wametenga fungu kwa ajili ya kuvikarabati vituo hivyo hasa maeneo ya mijini, ili kuyawezesha magari ya zimamoto yanapoishiwa maji kuyapata umbali wa mita 100 mjini na umbali wa mita 200 vijijini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga amesema jeshi hilo linahitaji vituo 98 vya kujazia maji kwenye mikoa 11, kwani vilivyopo vimechakaa hivyo havifanyi kazi na kusababisha usumbufu na malalamiko kwa wananchi yanapotokea majanga ya moto.
Naye Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini amesema mtambo huo wa kuzima moto kwenye majengo marefu umekuja kwa wakati, kwani jiji hilo lilikuwa na uhitaji wa mtambo huo kutokana na majengo mengi marefu yaliyojengwa.
Jiji humo jengo refu ni la Kambarage Tower lenye ghorofa 11.