Wajumbe Bawacha walia na posho

Dar es Salaam. Muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) wajumbe wa mkutano huo wamepaza sauti ya kuhitaji posho zao kabla ya mchakato huo.

Hali hiyo inajiri muda mchache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwasili kwenye viunga vya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam kunapofanyikia mkutano mkuu wa uchaguzi wa Bawacha.

Mbowe alipofika alikwenda moja kwa moja kwenye chumba maalumu cha wageni akisubiri utaratibu kuingia ndani ya ukumbi wa mkutano.

Tukio hilo limetokea leo Alhamisi Januari 16, 2025 wakati wajumbe hao wakiwa ndani ya ukumbi, kila mara wanapopewa maelekezo na mshereheshaji, Devotha Minja kupunga mkono na kupiga vigelegele walipaza sauti wakidai posho…posho…

Katika kutuliza hali hiyo, Minja ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, amewaahidi mambo hayo ni madogo kwani chama hicho  ni taasisi kubwa haishindwi kwa mambo madogo kama hayo. Hata hivyo, baada ya muda mfupi hali hiyo ilirejea kawaida.

Kwa sasa hali imetulia kidogo na wajumbe hao wametakiwa kuwa watulivu kujiandaa kuwapokea wageni waalikwa na wanatakiwa kuonyesha ushirikiano kwa kila kiongozi atakayeingia kwa sababu wao ni walezi.

Hali ya kudai posho ilijitokeza pia katika mkutano mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) uliofanyika Januari 13, 2025 ukumbini hapo.

Wajumbe wa mkutano wa Bavicha walidai licha ya kuahidiwa na viongozi kuwa watapata fedha zao lakini ilikuwa kinyume, jambo lililowafanya baadhi yao kutoka nje ya ukumbi kabla ya kubembelezwa kurejea tena.

Lissu, Mbowe walivyopokelewa

Shangwe na vigelegele vilisikika baada ya Lissu kuingia ndani ya ukumbi, ambaye alikwenda kuketi moja kwa moja kwenye meza kuu na kuanza kuwachezesha wimbo wa chama uliokuwa ukipigwa.

Wajumbe walisikika wakisema Lissu licha ya mshereheshaji kuwatuliza, lakini waliendelea kutaja jina la Lissu… Lissu

Muda mchache baada ya Lissu kuingia akafuata Mbowe ambaye alitandikiwa khanga ikiwa ni ishara ya upendo kwa mwenyekiti huyo ambaye anawania nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Baadhi ya makada na wajumbe wa mkutano walijipanga mlango kwa mistari miwili wakiwa na mabango yenye picha yake.

Mbali na hilo, Mbowe akiambatana Ezekia Wenje anayewania umakamu mwenyekiti bara, amesindikizwa na matarumbeta yaliyokuwa yakipigwa mdundo wimbo wa Chadema wa ‘people’s power’ people’s power’.

Wanawake walikwenda mbele ya jukwaa kuu na kuanza kucheza nyimbo za chama hicho, huku Mbowe na Lissu nao wakiimba na kucheza wakiwa wamesimama mbele ya  kwenye viti vyao.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari mbalimbali

Related Posts