‘Fanyeni utafiti ughaibuni kujifunza mambo mapya’

Iringa. Mwenyekiti wa Chama cha Historia Tanzania na Mdhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Maxmilian Chuhula amesema ipo haja kwa wasomi wa vyuo vikuu kufanya utafiti nje ya nchi, ili mbali ya kuongeza maarifa, wajifunze tabia na desturi mataifa mengine.

 Amesema ni rahisi wasomi hao kuja na maandiko yatakayosaidia kuikomboa jamii kutoka kwenye changamoto mbalimbali, ikiwa utafiti utafanywa kwa ubunifu na weledi.

Dk Chuhula amesema hayo jana Aprili 19, 2024 wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa kitabu kinachohusu matarajio ya utengamo wa Afrika, mgogoro wa Sahara, ambacho utafiti wake umefanyika kwenye nchi tofauti ikiwamo Morocco.

Kitabu hicho kilichochapishwa na Africa Proper Education Network (APE), kimeandikwa na Dk Chuhila akishirikiana na mhadhiri mwingine wa UDSM, James Zotto.

 “Fanyeni utafiti nje ya Tanzania mjifunze vitu vingi, mjifunze kuhusu watu wengine wa Afrika na muongeze maarifa.

“Kitabu hiki kinauhalisia na naamini mkikisoma kitawaongezea maarifa ya kutosha kuhusu utengamano wa Afrika hasa mgogoro wa Sahara Magharibi,” amesema.

Amesema kitabu hicho kitakuwa miongoni mwa vitabu vitakavyowapatia wanafunzi uelewa mpaka kuhusu masuala ya utengamano waAfrika, hasa mgogoro wa Sahara Magharibi.

Dk Chuhila amesema licha ya kuwa na maandiko mengi, kitabu hicho ni cha kwanza kwenye safari yao kitaaluma.

Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU), DK Makungu Bulayi amewataka wanafunzi kujenga tabia ya kusoma vitabu na kujikita katika uandishi, ili kufikia malengo yao kitaaluma.

Amesema uzinduzi wa kitabu hicho umekiheshimisha chuo chao hasa wakati huu wa utandawazi ambao, wanafunzi wanapaswa kujifunza mambo mengi zaidi kwa kusoma vitabu vilivyoandikwa na wanazuoni tofauti.

“Wekezeni kwenye kuandika vitabu, maandiko yana nguvu kubwa. Someni vitabu na wekezeni kwenye kuandika,” amesema Bulayi.

Baadhi ya wanafunzi wa RUCU, wamesema ujio wa kitabu hicho chuoni kwao utawapa mwanga mpana hasa wale waliojikita kwenye masuala ya historia.

 “Tumepata mwanga mkubwa sana kwa ujio wa kitabu hiki zaidi, tumejifunza kwamba tunaweza kufanya tafiti hata nje ya Tanzania,” amesema Daud Daud, mwanafunzi wa RUCU.

Related Posts