Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu 15, akiwamo Mussa Zacharia (28), mkazi wa Kijiji cha Kanyegere, Wilaya ya Rungwe kwa tuhuma za kuiba mifuko 1,253 ya unga wa sembe iliyokuwa ikisafirishwa kwenda Malawi.
Tukio hilo limetokea jana Jumatano, Januari 15, 2025, saa 2:00 asubuhi baada ya lori lenye namba za usajili LA 10214 aina ya Freight Liner kupinduka katika Mlima Kanyegele, likiwa na mifuko ya unga wa sembe yenye uzito wa kilogramu 25 kila mmoja.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akizungumza leo Alhamisi Januri 16, 2025 ofisini kwake jijini Mbeya, amesema lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Damson Vicent (35), mkazi wa Lilongwe, Malawi, alipata majeraha madogo.
Amesema lori hilo lilikuwa likisafirisha shehena ya unga kutoka Mbeya kwenda Lilongwe na lilipofika kwenye mteremko mkali wa Mlima Kanyegele, lilipoteza mwelekeo na kupinduka.
“Baada ya ajali hiyo, badala ya wananchi wa vijiji jirani kusaidia kuokoa mali, walitumia fursa hiyo kuiba unga kwa kutumia usafiri wa pikipiki. Polisi walianza msako mara moja na kumkamata Mussa Zacharia na wenzake 14 wakiwa na vielelezo, ikiwamo mifuko 65 ya unga, minne kati ya hiyo ilikuwa tayari imepunguzwa ujazo,” amesema kamanda Kuzaga.
Amesema watu hao pia, wamekamatwa na turubai mbili za lori lililopata ajali pamoja na pikipiki saba zilizokuwa zikitumika kusafirisha unga huo,” amesema.
Kamanda Kuzaga amesisitiza kuwa, msako wa wahusika wengine unaendelea, huku akibainisha kuwa tamaa ya kujipatia kipato kwa njia za mkato ndiyo chanzo cha tukio hilo.
Amewaonya wananchi wanaoishi karibu na barabara kuu kuepuka kutumia ajali kama fursa ya kufanya uhalifu, bali washirikiane kufanya uokozi ili kuepuka mkono wa sheria.
Mkazi wa Kiwira, Stella Mwakyangwe amepongeza jitihada za polisi kuwabaini wahalifu haraka.
“Sisi tunaokaa jirani na barabara, tunaona magari hata madogo yakipata ajali, vijana wengi badala ya kuwasaidia waliokuwa kwenye magari, wanakimbilia kuiba vitu, hili liwe fundisho,” amesema Mwakyangwe.
Mkazi mwingine, Doto Mwampashi amesema kitendo cha polisi kuwasaka watu waliopora mali kwenye ajali ni cha kupongezwa.
“Vijana wengine wanakaa barabarani kwa wakisubiri ajali zitokee halafu wakapore mali badala ya kuokoa watu, hii ni dhambi kubwa,” amesema Mwampashi.