JANA Tanzania imewakilishwa vyema na staa wa zamani wa Taifa Stars, Mrisho Ngassa kule Nairobi, Kenya kulikokuwa na droo ya fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) 2024.
Mbele ya uso wa luninga hapa mtaani kwetu tukamuona Mrisho Ngassa akiwa na suti yake maridadi nyeusi akichezesha droo ya Chan ambapo Tanzania ‘Taifa Stars’tukaangukia kundi B.
Kulia kwake alikuwapo kiungo kiraka mstaafu wa Uganda, Hassan Wasswa Mawanda aliyewahi kucheza soka la kulipwa Uturuki na Saudi Arabia.
Kushoto kwa Ngassa kukawepo kiungo mmoja wa shoka wa zamani wa Inter Milan na timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars MacDonald Mariga ambaye kwa sasa ni makamu wa rais wa shirikisho la mpira wa miguu Kenya (FKF).
Ngassa hajaenda pale kwa kupendelewa bali kama mmoja wa magwiji wa Taifa Stars kwani anashikilia rekodi mbili alizoweka akiwa na jezi ya timu hiyo ambazo hata akiwa Yanga, Simba au Azam hakuwahi kuziweka.
Ameteuliwa kwa vile ndio mchezaji aliyecheza idadi kubwa ya mechi za Taifa Stars na wakati huohuo Ngassa ndio mfungaji bora wa muda wote wa timu yetu ya taifa akiwa na mabao 25.
Uteuzi wa Ngassa kupewa fursa ya kushiriki na kuchezesha droo ya mashindano makubwa kama Chan ni matunda ya jasho ambalo alikubali kuvuja kwa ajili ya Taifa Stars pamoja na kwamba kizazi chake hakikufanikiwa kupata mafanikio kama ambavyo hiki cha sasa kinapata.
Kumbe inawezekana wachezaji wetu wa sasa wakapandishwa chati na hadhi na Taifa Stars ikiwa wataitumikia kwa kujitolea kama ambavyo wanafanya katika klabu zao kama ambavyo Ngassa alikuwa anafanya.
Muda wa kujitathmini bado wanao kama wataanza kuwa tayari kuipigania jezi ya Taifa Stars au waendelee kuona ni kama timu ya kuzugia.