Sunzu, maveterani kuchangia madogo wenye saratani

WACHEZAJI wa zamani wa klabu mbalimbali jijini Mwanza wameandaa tamasha la michezo ya kirafiki katika mchezo wa soka na netiboli, ili kuchangisha fedha za kusaidia mahitaji mbalimbali ya watoto wenye saratani wanaotibiwa na kuishi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na klabu ya Mwanza Veterani inayojumuisha wachezaji mbalimbali akiwamo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Felix Sunzu raia wa Zambia, litafanyika Februari 15, mwaka huu jijini Mwanza.

Kwa upande wa soka, timu za maveterani za Mwanza SC, Pamba, Bugando FC, Mwanza Stars, Charity Sports, Nyegezi na Watumishi zitamenyana, huku katika netiboli kuna Mwanza Veterani na Bugando Netiboli pamoja na nyingine mbili ambazo hazijathibitisha zikitarajiwa kuchuana.

Katibu wa Mwanza Veterani, Simon Sinkala aliliambia Mwanaspoti lengo ni kurudisha shukrani kwa jamii kwa kusaidia watoto zaidi ya 30 wenye saratani wanaotibiwa hospitali ya Bugando ambao wanaishi hosteli bila ndugu, chakula na mahitaji mengine.

“Bonanza letu linalenga kufanya mchango wa kupata mahitaji ya watoto wenye saratani, tunaomba wadau washiriki. Atakayeguswa atauona uongozi wetu kupata utaratibu wa kufikisha msaada wake kwa watoto hao,”  alisema Sinkala.

Daktari Idara ya Saratani Hospitali ya Bugando, Richard Mhone alisema kwa mwaka wanapokea wagonjwa wapya wenye saratani 250 hadi 350 ambao ni watoto, huku hospitali hiyo ikiwasaidia kuishi kwenye bweni wagonjwa wanafika bila ndugu, sehemu ya kulala na chakula bure.

“Wagonjwa wetu wana mahitaji ya vitu vya kawaida tu vya nyumbani kama chakula, mafuta ya kula, ya kupaka, dawa za meno na pampasi kwa watoto. Wanapopata vitu hivyo inawasaidia kubaki kwenye ule mtiririko wa matibabu ambao sisi tunakuwa tunauhitaji,” alisema Dk Mhone

Mdau wa Mwanza Veterani, Abdul Said ‘Mambo ya Fuso’ alisema bonanza hilo ni mwendelezo wa klabu hiyo kushiriki katika changamoto za jamii inayowazunguka, huku akiahidi kuwa baada ya hapo watafanya ziara ya michezo visiwani Zanzibar Mei, mwaka huu kudumisha mahusiano na utalii.

Related Posts