Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka viongozi wapya wa mabaraza na watakaochaguliwa kuhakikisha chama hicho, kinajibu changamoto za kijamii na wananchi, siyo masuala yanayohusu siasa pekee.
Mbowe anayewania nafasi ya uenyekiti kwa mara nyingine baada ya kukiongoza chama hicho kwa miaka 21, amesema kuna programu ya Chadema Family ambayo haijafanikiwa kwa sababu haikupewa umuhimu mkubwa, hivyo kuanzia sasa ipewe kipaumbele katika uongozi mpya.
“Yeyote atakayeingia kuongoza chama, kwenye chama na mabaraza ahakikishe tunakwenda kuhuisha uwepo wa Chadema family katika kaya moja moja. Kila Mwanachadema atambue katika kuhusika kuijenga na kuiboresha jamii.
“Kila mwanachama wa Chadema atambue yeye ni bega la kumlilia Mwanachadema mwenzake anayefikwa na matatizo katika maeneo yake. Tunataka Wanachadema wote mbali na majukumu yenu ya kisiasa, tujipe majukumu ya kuilea jamii,” amesema Mbowe.
Mbowe ameeleza hayo leo Alhamisi Januari 16, 2025 wakati akifungua mkutano mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) ambapo pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya kuwachagua viongozi watakaoongoza baraza hilo hadi mwaka 2029.
Maelekezo yamekwenda kwa vijana (Bavicha), wazee (Bazecha) na wanachama wa chama hicho kwa ujumla.
Akiendelea na hoja kuhusu umuhimu wa Chadema kuwa karibu na jamii, Mbowe amesema: “Kila mtaa mmoja wenye tawi la Chadema basi, Wanachadema wote wanakuwa familia, ikitokea mmoja wetu amefikwa na msiba au ugonjwa, tunapaswa kuungana na kushikana mikono, tukamsaidie kupika, kubeba mahema.”
“Iwe ni marufuku kwa Mwanachadema yeyote kuona mwenzake anapata shida, kuona shida hiyo haimuhusu, shida ya Mwanachadema ni shida yetu wote. Tusisubiri kuwa chama cha uchaguzi, bali tuwe ni chama kinachoishi maisha ya kila siku ya wana jamii na nyie kina mama mkiamua kuchukua wajibu huo, chama hiki kitakuwa cha tofauti,” amesema Mbowe.
Amesisitiza Chadema kwa sasa halitakuwa chama cha kusubiri uchaguzi, kwa sababu wananchi wa kawaida wanaona vyama vya siasa ni vyombo vya uchaguzi, lakini hivi sasa chama hicho kikuu cha upinzani kitakuwa kimbilio la wananchi.
“Wananchi wasio Wanachadema wakiona Wanachadema wanasaidiana kuzikana, wanachangiana matibabu, wanachangiana kwenye shida la raha, hakika wataona umuhimu wa kuja Chadema na maisha hayatakuwa ya siasa bali ya kusitiri jamii yetu katika kila nyanja zikiwamo za kiuchumi, kijamii na kisiasa,” amesema Mbowe.
Mbowe amesema uimara wa baraza hilo hautapatikana kwa mikutano mikuu yenye mbwembwe bali mipango na mikakati madhubuti ya kina mama wengi kuanzia ngazi ya kaya, vijiji na vitongoji.
Amewataka viongozi wapya watakaochaguliwa kuhakikisha wanaijenga Chadema ngazi ya chini, siyo kukijenga kwenda juu, akisema mara nyingi Chadema inaonekana ni watu.
Mbowe alitumia nafasi hiyo, kuwataka wajumbe wa mkutano mkuu na wagombea baada ya uchaguzi huo kuisha washikane mikono, akisema kila atakayeshinda kuacha kiburi cha ushindi.
“Lazima tutoke Dar es Salaam tukiwa tumeshikana mikono kuliko ilivyokuwa kawaida yetu. Tunataka Bawacha isijitafsiri kama baraza la viti maalumu, ndugu zangu narudia tena, tusiingie na kuijenga Bawacha kwa sababu ya ndoto ya ubunge na udiwani wa viti maalumu, kila mmoja aingie kwenye baraza hili kwa dhamira ya kuijenga jamii ya Watanzania,” amesema Mbowe.
Awali, Kaimu Mwenyekiti wa Bawacha, Sharifa Suleiman amesema siku ya uchaguzi imemtafakarisha namna watu walivyohoji Uzanzibar wake wakati akihudumu kwenye nafasi hiyo, wengi wakitabiri namna atakavyoua baraza hilo.
Sharifa ametaja nyakati hizo hazikuwa rahisi kwake akikumbuka mengine ndani ya uongozi wake, hasa wabunge 19 wa viti maalumu walivyokwenda kuapa bungeni bila ridhaa ya chama hicho.
“Ni kipindi ambacho kilikuwa na kiza kinene kila mmoja wakati huo alipitia misukosuko kwa wakati wake na sasa nina furaha kuona meli hii ya wanawake imefika inapotakiwa ikiwa salama, sasa wanawake tuna faraja na imani kwa chama,” amesema.
Kuhusu changamoto zilizopo Bawacha, Sharifa amesema ipo migogoro ambayo imetatuliwa na mengine hayajatatuliwa, akisema wanachokifanya sasa ni kuendelea kuhimizana kustahimiliana kwa sababu wanajenga nyumba moja.
“Dhumuni ni kujenga Bawacha kuwa kimbilio la wanawake wote wa Tanzania, na pale wanapopata changamoto baraza hilo liwe kimbilio lao.
“Bawacha itaendelea kufungua milango kwa makundi yote ikiwemo wakulima wafanyabiashara, wanazuoni, watumishi wa umma, wazee na vijana kuendelea kulinda haki,” amesema Sharifa ambaye alijiuzulu wadhifa huo baada ya kumaliza hotuba yake.
Sharifa amejiuzulu nafasi hiyo kwa sababu yeye ni mgombea uenyekiti wa Bawacha akichuana na Suzan Kiwanga, Celestina Simba katika uchaguzi utakaofanyika leo baadaye.