Dar es Salaam. Hatimaye wajumbe wa mkutano mkuu wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), wameanza kulipwa posho zao walizokuwa wakishinikiza kulipwa kabla ya kuanza mkutano huo asubuhi.
Mapema asubuhi leo Alhamisi Januari 16, 2025 wajumbe hao walipaza sauti wakitaka kulipwa posho zao ikiwemo nauli kulingana na mikoa wanayotoka.
Asubuhi muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa Bawacha unaofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam kuwachagua viongozi wakuu wa baraza hilo wajumbe walipaza sauti ya kuhitaji posho zao kabla ya mchakato huo.
Hali hiyo ilijiri muda mchache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwasili kwenye viunga hivyo na kwenda moja kwa moja kwenye chumba maalumu cha wageni akisubiri utaratibu kuingia ndani ya ukumbi wa mkutano.
Hata pale mshereheshaji wa tukio hilo, Devotha Minja alipojaribu kuwatuliza na kuwaahidi kuwa hayo ni mambo madogo kwani Chadema ni taasisi kubwa haishindwi kuwalipa, hawakuelewa.
Kuanzia saa tisa jioni baada wajumbe kupata chakula cha mchana katika pitapita kwenye viunga vya korido za ukumbi wa Ubungo Plaza, Mwananchi imeshuhudia wajumbe hao wakiitwa kikanda kwa ajili ya kuchukua posho zao zilizokuwa zinatolewa katika maeneo tofauti.
“Wajumbe wa kanda ya ziwa na magharibi naombeni ingieni ukumbi mkubwa wale wengine wakiwemo wa Tanga njooni huku,” walisikika waratibu wakitoa maelekezo hayo.
Mmoja wa wajumbe jina tunalihifadhi amethibitisha kuitwa kwa ajili kupokea posho” nimeitwa ndiyo nakwenda kuchukua posho yangu,” amesema mjumbe huyo aliyeonekana na furaha.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi