Uru Shimbwe walia ubovu wa barabara

Moshi. Wananchi wa Kata ya Uru Shimbwe, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara ya Mamboleo – Shimbwe, hali ambayo imekuwa ikiwapa changamoto kubwa ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda masokoni kipindi cha mvua.

Wananchi hao wanaojishughulisha na kilimo cha ndizi, viazi pamoja na matunda kama  pasheni, parachichi na maembe wameiomba Serikali kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa barabara hiyo na kuiwezesha kupitika kipindi chote cha mwaka.

Wamesema ujenzi utarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Meneja Wakala wa Barabara za vijijini na Mjini (Tarura) Wilaya ya Moshi, Orota Africano amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 10.3, iko kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango  cha changarawe na  kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imetengewa bajeti ya Sh100 milioni na kwa sasa wanasubiri idhini ili waweze kuitangaza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, leo Januari 16, 2025, baadhi ya wananchi wa kata hiyo, wamesema barabara hiyo imekuwa changamoto kubwa ambapo ahadi za kuitengeneza zimekuwa zikitolewa na viongozi wa Serikali mara kadhaa bila utekelezaji, hali ambayo imekuwa ikiwasababishia usumbufu na gharama kubwa za usafiri.

Kandida Tesha mkazi wa kijiji cha shimbwe Juu amesema ubovu wa barabara hiyo umechangia kupanda kwa gharama za maisha kwa kuwa hulazimika kutumia fedha nyingi za usafiri hasa kipindi cha mvua.

” Wajawazito wakipata uchungu kuwapeleka hospitali kujifungua wanateseka sana wanatumia bodaboda tena kwa shida, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa maisha yao na mtoto” amesema Tesha

John Leonard muhudumu wa afya ngazi ya jamii kata ya Uru Shimbwe amesema, “tangu mwaka 1961 tupate uhuru mpaka sasa barabara hii ya Uru Shimbwe imekuwa ni tatizo kubwa, wakati wa mvua za masika haipitiki kabisa na ni hatari huko tunakoelekea inaweza ikasababisha ajali kubwa na watu wakapoteza maisha.

Amesema, “kumpeleka mgonjwa hospitali ni changamoto kubwa, wakati mwingine tunalazimika kubeba wagonjwa kwa chekecheke wakati wa mvua kutokana na kukosekana kwa vyombo vya usafiri kwa sababu ya utelezi, hili ni tatizo kubwa, Serikali iliangalie kwa jicho la tofauti”.

Jackline Nelson amesema kutokana na ubovu wa barabara hiyo, kipindi cha mvua wanatumia hadi Sh10,000 kutoka Uru hadi Moshi mjini gharama ambayo ni kubwa ikilinganishwa na hali zao za kiuchumi.

Amesema, “haiwezekani tuko Moshi halafu hatuna barabara, huku kwetu tuna maporomoko ya maji ya Mnambe na watalii wengi huwa wanakuja lakini wakati wa mvua tunapoteza mapato, pia tunalima matunda mbalimbali, ndizi na kina mama wanateseka kubeba kwa kichwa hadi Moshi mjini kutafuta masoko kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Diwani wa Kata ya Uru Shimbwe, Bertin Mkami amesema barabara hiyo iliahidiwa kujengwa na Serikali kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa imejengwa Kilomita 1.5 pekee.

Related Posts