Wezi wavamia waiba kichanga | Mwananchi

Kibaha. Watu ambao hawajafahamika wamevamia nyumbani kwa mkazi wa Kibaha kwa Mfipa Mkoa wa Pwani Melkisedeck Sostenes na kupora gari, pesa na vitu mbalimbali kisha kuwatumbukiza wamiliki wa nyumba kwenye chemba za vyoo.

Watu hao wanaodaiwa kutekeleza tukio hilo saa 12 asubuhi pia wanadaiwa kuondoka na mtoto mchanga mwenye umri wa miezi saba ambaye ni wa wanandoa hao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Alhamisi Januari 16, 2025 mmiliki wa nyumba hiyo Melkisedeck Sostenes amesema kuwa watu hao walifika nyumbani kwake jana saa 12  asubuhi na walimvizia alipokuwa akitoka ndani kwenda kulisha kuku bandani.

 “Kwa kawaida huwa naamka saa 12 asubuhi  ili kulisha kuku,  sasa jana nilipotoka na kufika mlangoni watu wanne wakaja kwa nyuma na kuniamuru nisipige kelele wakitaka niende nao ndani kuwapa pesa” amesema

Amesema kuwa alijaribu kupiga kelele za kuomba msaada lakini alibanwa na kupigwa ubapa wa panga kisha kuingizwa ndani na kutakiwa kuonyesha pesa zilipo pamoja na simu zote zikiwemo za uwakala wa huduma za pesa na zile za matumizi ya kawaida.

“Baada ya kuingia nao ndani wakasema twende chumbani unakolala ili utupatie pesa wakaanza kusachi na wakachukua pesa simu zangu nne na wakanilazimisha kwa vitisho kuwa niwapatie namba za siri za kuhamisha pesa kutoka kwenye simu zangu kwenda kwenye simu nyingine, sikuwa na namna nikawatajia namba za siri amesema.

Amesema baada ya kumaliza hatua hiyo walichukua vifaa mbalimbali vya ndani pete ya ndoa kisha wakaondoka naye kuelekea nje ambako walichukua kuku waliokuwa ndani ya banda na kuomba ufunguo wa gari lake kisha kupakia vitu hivyo ndani ya gari.

“Tulipofika nje wakanipeleka kwenye chemba la choo wakanifunga kamba miguuni na mikononi wakaanza kunitumbukiza kwenye shimo hilo kutokana na unene wangu waliponitumbukiza huku wamenifunga kamba mikononi nilikwama wakanifungua kamba mikononi” amesema.

Amesema kuwa baada ya kumfungua kamba mikononi walimshika na kumtumbukiza kwenye shimo hilo la choo kwa shida na alipokwama walimshindilia kwa kutumia miguu hali iliyosababisha kufika chini ndani ya shimo hilo akiwa na maumivu makali.

“Nilifika ndani ya shimo wakati wako nje niliwasikia wakibishana kuhusu mtoto wengine wakishauri kuwa wamuache huku wengine wakitaka waondoke naye, baadaye sauti zikapotea na walifunika shimo juu wakaweka nyasi,”amesema.

Amesema kuwa baada ya kumuacha ndani ya shimo walirudi ndani na kumchukua mkewe aitwae Johari Bung’ombe ambaye pia walienda naye hadi nyumba ya jirani ambayo kwa sasa watu hawaishi humo wakamtumbukiza kwenye shimo la choo.

“Sijui nia yao wale watu maana baada ya kunitumbukiza mimi kwenye shimo la choo la kwetu walienda kwa mke wangu wakamchukua na kwenda kumtumbukiza kwenye shimo kama walivyofanya kwangu “amesema.

Amesema kuwa tangu 12 alikaa ndani ya shimo hilo hadi saa 4 asubuhi baada ya kuokolewa na dereva bodaboda aliyefika nyumbani kwake kumuuliza kwa kuwa waliona amechelewa kufungua duka.

“Wakati niko ndani ya shimo niliendelea kugonga mabomba yanayoingiza maji taka huku nikipiga kelele za kuomba msaada bahati nzuri huyo dereva bodaboda alifika na kusikia kisha akaita watu wengine ndio kuja kuniokoa” amesema.

Amesema kuwa baada ya kutoka nje aliwaeleza majirani zake habari hiyo kisha wakaanza msako wa kutafuta mkewe na mtoto na baadaye kutoa taarifa polisi.

“Tulianza kuwatafuta mke wangu na mtoto kuanzia saa 4 asubuhi  hadi saa 11 jioni ndipo tuliposikia sauti kwa mbali ikitokea ndani ya shimo la choo kwa jirani na tulipofika tuliona na tukamuokoa na mpaka sasa yuko hospitali anaendelea na matibabu.”

“Lakini hatujui  mtoto wetu alipo na yuko na hali gani tunamuomba Mungu amlinde mtoto wetu ili tumpate akiwa salama” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Galagaza, Saidi Siasa amesema kuwa amepokea kwa masikitiko tukio hilo huku akiamini kuwa kutokana na nguvu na uwezo wa Polisi watuhumiwa hao watapatikana.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo leo Januari 16,2015 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,  Salim Morcase amesema kuwa wamepata taarifa na wanaendelea na uchunguzi.

Related Posts