Wanaodaiwa kusafirisha kilo 1500 za bangi, wanaendelea kusota rumande

Dar es Salaam. Serikali imesema uchunguzi unaendelea katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 1350, inayomkabili Mohamed Bakari (40) na wenzake, Suleshi Mhairo (36).

Wakili wa Serikali, Titus Aron ametoa maelezo hayo, leo Januari 16, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantua Mwankuga wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Aron amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na hivyo anaomba mahakama ipange tarehe nyingine.

Hakimu Mwankuga ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Januari 3, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa Novemba 12, 2024, eneo la Nyakwale lililopo Kigamboni, kwa pamoja wanadaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 1350, wakati wakijua ni kosa kisheria.

Katika hatua nyingine, upelelezi wa kesi ya kusafirisha kilo 151.43 za bangi inayomkabili mkazi wa Chanika Buyuni, Idd Mohamed Idd (46) haujakamilika.

Wakili Aron ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mwankuga wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Kutokana na hali hiyo, hakimu Mwankuga aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi hiyo, Idd adaiwa kutenda kosa hilo Novemba 13, 2024 katika eneo la Pweza lililopo Sinza C, wilaya ya Kinondoni.

Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa alikutwa akijihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa Kilo 151.43 kinyume cha sheria.

Kesi hizo zimeendeshwa kwa njia ya video huku washtakiwa hao wakiwa rumande.

Hata hivyo, kiasi hicho cha dawa kinachowakabili washtakiwa wote, kimewafanya wakose dhamana na hivyo wataendelea kubaki rumande.

Related Posts