Dar es Salaam. Matarajio ya Watanzania juu ya bima ya afya kwa wote kuanza Julai mosi mwaka huu ‘yameota mbawa’ baada ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2024/2025 yaliyowasilishwa jana bungeni kutoonyesha mwelekeo wa kuanza hivi karibuni.
Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ulipitishwa na Bunge la Novemba mwaka jana kabla ya kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sheria kamili Desemba Mosi 2023 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
Kabla ya kupitishwa na Bunge, muswada huo ulikwama mara kadhaa baada ya wabunge na Spika wa Bunge hilo, Dk Tulia Ackson kuonyesha shaka kwenye baadhi ya vifungu vya muswada huo, hasa vyanzo vya fedha kwa wasio na uwezo wa kuchangia.
Muswada uliporudi bungeni kwa mara nyingine, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitaja vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyogharamia watu hao wasiojiweza.
Vyanzo alivyovitaja na Bunge likaupitisha ni mapato yatokanayo na vipodozi, vinywaji vikali, michezo ya kubahatisha, vinywaji vyenye kaboni, mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki, fedha zitokanazo na Bunge, mapato yatokanayo na uwekezaji wa mfuko, zawadi na misaada kutoka kwa wadau.
Hata hivyo, jana akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, Waziri Ummy amesema Sh6 bilioni zimetengwa kutekeleza afua sita ikiwemo bima ya afya kwa wote, kwa kuanzisha mchakato wa mfumo wa utambuzi na elimu.
Akifafanua zaidi matumizi ya fedha hizo, amesema, “kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote nchini, ikiwemo mfumo wa utambuzi wa wanufaika pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya,” amesema Ummy na kuongeza fedha hizo pia zitaimarisha uhai na ustahimilivu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Hilo linaashiria huduma za matibabu kwa wote kwa kutumia, haitaanza mwaka ujao wa fedha hali iliyoamsha wananchi mbalimbali waliokuwa na matarajio ya kuanza kunufaika na huduma hiyo.
Mkazi wa Toangoma jijini Dar es Salaam, Farida Sekela amesema imani yake baada ya Rais kutia saini na kuwa sheria ilikuwa ianze kazi.
“Matarajio yangu ilikuwa wakati huohuo ianze kufanya kazi, huwa tunasikia sheria ikishasainiwa na Rais inaanza kutekelezwa, kila Mtanzania anahitaji huduma bila kikwazo cha fedha. Tulishakubaliana na tulipigiwa kelele na Serikali inasema tujiunge, huo upembuzi yakinifu ni matumizi mabaya ya fedha,” amesema Farida.
Miongoni mwa wazazi waliozungumza na Mwananchi Digital, waliweka wazi kuwa baada ya kukosekana kwa Toto Afya Card iliyoondolewa katika vifurushi vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), matarajio yao yalikuwa ni bima ya afya kwa wote.
“Mwaka sasa umeisha bado hatujapata suluhisho. Tulisubiri bima ya afya kwa wote tukiamini tutaanza kupata huduma nafuu ifikapo Julai mosi, hili la mfumo wa utambuzi limetuchanganya,” alMEsema Michael Raphael, mkazi wa Arusha.
Licha ya maoni hayo, taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi kuhusu makadirio ya bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni jana na Stanslaus Nyongo, mwenyekiti wa kamati hiyo, ilisisitiza vyanzo vya fedha.
“Kamati inaendelea kusisitiza, Serikali ikamilishe mchakato wa kufanya tathmini ya vyanzo na viwango vya fedha, kwa ajili ya mfuko wa kugharamia watu wasio na uwezo kupitia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote,” amesema.
Mjumbe wa Kamati Kuu na Msemaji wa sekta ya afya ACT- Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga amesema licha ya ucheleweshwaji wa kuanza kwa mchakato huo, mfumo mzima wa matumizi ya ugharamiaji huduma za afya umecheleweshwa.
“Hata kama sheria hii ilianza kufanya kazi, bado hatutatui changamoto yoyote ya ugharamiaji huduma za afya. Haimpi unafuu Mtanzania bali inalazimisha wengi walipie gharama kubwa kupata huduma za afya,” amesema Dk Sanga.
Wakati wadau wakisema hayo, Mkufunzi wa Chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii (ACISP), Anselim Anselim amesema katika mchakato wa utekelezaji wa sheria hiyo, kuna mchakato wa upembuzi yakinifu ambao Wizara ya Afya inatakiwa ifanye kama maandalizi ya huduma.
Amesema mchakato huo unatakiwa kufanywa kwa umakini mkubwa, kwani tayari vifurushi vilileta shida, hivyo kuna utafiti unatakiwa kufanywa na wataalamu ili kuandaa mfumo.
“Mchakato wa bima ya afya ya pamoja una mambo mengi, siyo rahisi, kuna mengi yanatakiwa kufanyika. Pia lazima tujifunze kwa wenzetu waliofanikiwa walifanya kwa namna ipi, ikaleta matokeo chanya,” amesema Anselim.
“Wenzetu Rwanda asilimia 90 wapo kwenye mfuko wa pamoja wa afya, lakini kwa sasa mfuko wao unaanza kutetereka, ni suala gumu kidogo. Ukiangalia Ujerumani wametumia miaka 147 kufikia asilimia 100 ya wenye bima za afya, walianza tangu mwaka 1887,” amesema Anselim.
Hata Mwenyekiti wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Tanzania (Aphtha), Dk Egina Makwabe amesema mchakato ambao wizara inaanza nao ni muhimu na ametahadharisha, kuwa huenda mchakato wa bima ya pamoja kwa wote utaanza baada ya uchaguzi wa mwaka 2025.
“Ni dalili nzuri naiona lakini katika mchakato wa kutoa elimu na kukusanya maoni sekta binafsi tumekuwa tukisahaulika, wanakuja mwishoni wakituambia tekelezeni hili, ilhali tuna mchango mkubwa, watoaji wa huduma Dar es Salaam asilimia 80 wanatoka sekta binafsi na Serikali ni asilimia 20 pekee.
“Ukituacha nje unakuwa hujaitendea jamii haki, hivyo inataka ijumuishe wote sekta binafsi, umma, mashirika ya dini yahusishwe pia,” amesema.
Akizungumzia hilo, Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema mchakato huo unalenga kutambua nani anastahili kuingia katika ruzuku na nani hastahili.
“Kuna kazi ya kuwapata asilimia 26 wasio na uwezo lakini pia kufikisha elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wafanyakazi wa Serikali, sekta binafsi, wakulima, wafugaji, wavuvi kila jamii kwa namna yake,” amesema.