Mastaa Simba wana jambo lao Kwa Mkapa

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Kundi A katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku wachezaji wa timu huo wakitoa msimamo mzito kabla ya kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuvaana na CS Constantine ya Algeria.

Wachezaji hao wamekiri wanajua watalikosa vaibu la mashabiki kutokana na kufungiwa kuwaingiza katika mchezo huo wa marudiano dhidi ya timu hiyo ya Algeria, lakini wanamepania kuhakikisha wanaandika historia mpya ya kushinda kwa kushindo na kuongoza kundi hilo kabla ya kukomaa mechi za robo fainali.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wa timu hiyo, nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliliambia Mwanaspoti kuwa, wanatamani kumaliza kibabe mchezo huo wa Jumapili kwa kuongoza kundi kisha wapambane kwa kila hali ili kuvuka hatua ya robo na ikiwezekana kuandika rekodi mpya CAF.

Tshabalala alisema kila mchezaji wa Simba ana kiu ya kuandikwa majina yao katika historia ya klabu hiyo kwa kufanya makubwa kwa kuiwezesha timu ifike fainali za michuano hiyo, lakini wanajua hawawezi kufanikisha hilo kama hawataanza na mchezo huo wa mwisho wa Kundi A kisha kukomaa robo fainali.

“Tunacheza na timu ambayo inaongoza kundi, lakini tukishinda mchezo huo tutakuwa na pointi 13, tunahitaji kujipanga zaidi kuhakikisha inakuwa moja ya rekodi ambazo tunazitamani kwa msimu huu,” alisema Tshabalala anayecheza beki wa kushoto wa timu hiyo na Taifa Stars.

Kwa sasa Constantine inaongoza msimamo ikiwa na pointi 12, huku Simba ikifuata nyuma yao kwa alama 10, Bravos do Maquis ya Angola ikiwa ya tatu na pointi saba na CS Sfaxien ikiburuza mkia bila pointi yoyote licha ya kila moja kucheza mechi tano.

Simba ilifuzu kuifuata Constantine baada ya kutoka sare ya 1-1 na Bravos ugenini ambayo hata ikishinda dhidi ya Sfaxien ya Tunisia na kufikisha pointi 10 haitawasaidia kwa vile katika mechi dhidi ya Simba ugenini ilipoteza kwa bao 1-0 na hivyo kuzidiana ujanja wenyewe kwa wenyewe kundini humo.

Tshabalala alisema kutokana na msimamo ulivyo kwa sasa na kwa kikosi ilichonacho Simba ni wazi timu hiyo ina nafasi ya kufanya vitu vya ziada ili kufikia malengo wanayoyahitaji msimu huu katika michuano ya CAF ndio maana wachezaji wamepania kupambana kwa kila jasho ili kumaliza wababe wa kundi.

“Sio kitu kigeni kwa Simba kutinga robo fainali kwa sasa, tumeshafanya hivyo mara kadhaa nyuma, ila kiu tuliyonayo sasa tunasaka rekodi mpya zitakazokuwa zinazungumzwa na wadau wa soka ndani na nje ikiwamo kuvuka robo na hata ikiwezekana kucheza fainali na kubeba ubingwa,” alisema Tshabalala mmoja ya wachezaji waliotumikia timu hiyo kwa muda mfrefu akiwa na misimu 11 tangu mwaka 2014.

Kutinga mapema kwa robo fainali kwa Simba ni mara ya sita sasa katika misimu saba tangu iliporudi anga za kimataifa msimu wa 2018-2019, ambapo katika Ligi ya Mabingwa imeingia mara nne na misimu miwili ukiwamo huu imetinga kupitria Kombe la Shirikisho Afrika.

Related Posts