Geita. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita, kimekerwa na kasi ndogo ya ujenzi wa barabara za mradi wa Tactic zenye urefu wa kilomita 17 zinazojengwa kwa kiwango cha lami katika Manispaa ya Geita kwa gharama ya Sh22.5 bilioni ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB).
Barabara zinazojengwa ni Mkolani Mwatulole ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 18, Nyankumbu kivukoni (asilimia 28), Nguzo mbili-Samandito (asilimia 30), Imakengele –Mwabasabi (asilimia 6.5) na Mwatulole -Twiga ambayo ujenzi wake umefika asilimia 32.
Hata hivyo, Xie Fei ambaye ni Meneja wa Kampuni ya Sichuan Road Contractors&Bridige Gropup Corporation Ltd inayojenga barabara hiyo, amesema kilichokwamisha mradi huo ni mvua zinazoendelea kunyesha na changamoto ya fedha.
Fei amesema tayari ametafuta ufumbuzi wa fedha na sasa anasubiri mkopo kutoka Benki ya China.
Awali, mhandisi mshauri anayesimamia mradi huo, Isack Goodluck alisema ujenzi ulianza Novemba 2023 na unapaswa kukamilika Februari 19, 2025.
“Mradi wa Tactics mkataba ulisainiwa Septemba 2023 na ujenzi ulianza Novemba, umebakiza siku 40 mkataba umalizike na hadi sasa ujenzi ni chini ya asilimia 30,” amesema Goodluck.
Amesema kwa mujibu wa mkataba, mkandarasi huyo alilipwa malipo ya awali ya Sh3.3 bilioni ya kumuwezesha kuanza kazi.
Hata hivyo, Goodluck amesema kwa kazi aliyoifanya mkandarasi huyo hailingani na kiwango cha malipo ya awali ya Sh3.3 bilioni, hivyo Serikali haiwezi kuongeza fedha nyingine hadi pale atakapofanya kazi kulingana fedha aliyolipwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, Barnabas Mapande amemuomba Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kuingilia kati kuunusuru mradi huo.
Akizungumza baada ya kutembelea ujenzi wa barabara hizo, Mapande amesema chama kinasikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa ujenzi unaowakatisha tamaa wananchi.
“Tumepokea taarifa ya mradi huu, lakini nakosa neno la kuzungumza, ukisema sana unaweza kujikuta umetoa neno wengine wakaona umetukana, huu mradi unatia kichefuchefu, kila anayetoa taarifa lawama ni kwa mkandarasi kuwa na uwezo mdogo, sisi kama chama tunaomba taratibu za kisheria zichukuliwe maana muda wake umefika mwisho na ameshindwa kazi,” amedai Mapande.
Kuhusu mitambo, Goodluck amesema mkandarasi ameleta mitambo sawa na asilimia 57 ikiwamo ya kusaga kokoto, kuchanganya zege, jengo la ukandarasi pamoja na saruji na nondo lakini mradi huo umesuasua.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi amesema kwa mujibu wa mkataba, mkandarasi anapaswa kufanya kazi kisha kujaza ‘certificate’ ya malipo ili aweze kulipwa.
“Huyu mkandarasi kwenye nyaraka za kuomba kazi alidai anazo fedha, lakini kimsingi hadi sasa hajaingiza fedha na hajatimiza alichopaswa kufanya kwa mujibu wa mkataba, tayari mkandarasi mshauri amemwandikia kumwambia ameshindwa kutimiza matakwa ya mkataba,” amesema Myenzi.
Amesema kama watachukua hatua ya kumsimamisha kazi kwa sasa, Serikali inaweza kupata hasara kwa kutakiwa kumlipa.
Amesema kinachofanyika sasa ni kuendelea na mkataba kwa mujibu wa sheria na tayari mkandarasi huyo ameomba kuongezewa muda na ameshapatiwa maelekezo ambayo bado hajayafanyia kazi huku zikiwa zimesalia siku 40 akamilishe mradi huo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Uwanja, Joseph Musoma amesema hadi sasa kwenye mtaa wake nyumba tisa zimeharibiwa na maji kutokana na mkandarasi kujaza vifusi barabarani, hivyo maji ya mvua kukosa mwelekeo.