Dar es Salaam. Uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), umeingia siku ya pili, huku usiku wa kuamkia leo Ijumaa Januari 17, 2025 ukigubikwa na hekaheka za hapa na paleĀ ndani na nje ya ukumbi.
Imeshuhudiwa baadhi ya wafuasi wakitwangana ngumi kisha Jeshi la Polisi kufika kuimarisha ulinzi.
Bawacha ni baraza la mwisho la Chadema kufanya uchaguzi wake, baada ya la vijana (Bavicha) na wazee (Bazecha) kukamilisha mchakato huo, Januari 14, 2025 mwaka huu.
Baada ya uchaguzi wa Bawacha, utafuata uchaguzi wa chama kwa viongozi wa ngazi ya kitaifa, ikiwemo ya Mwenyekiti inayoshindaniwa na Tundu Lissu, Freeman Mbowe na Charles Odero.
Mara zote uchaguzi si lelemama, ndiyo yaliyoshuhudiwa hata katika mchakato huo wa Bawacha, ukihusisha vurugu na hatimaye ngumi.
Licha ya ulinzi mkali uliokuwepo lango kuu la Ukumbi wa Ubungo Plaza kuwa eneo gumu kufikika kwa asiye mjumbe halali, hiyo haikutosha kudhibiti purukushani.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, ugomvi wa ngumi ulizuka, ukianzia lilipo lango hilo lililojaa vijana wa ulinzi wa chama hicho.
Chimbuko la ugomvi huo ni mmoja wa watu aliyeamua kwenda katika lango hilo na kuwagomea walinzi walipomtaka aondoke.
Yalianza mabishano ya taratibu, ghafla yakawa kwa sauti ya juu, yakafikia kushikana mashati na hatimaye ngumi zikapigwa.
Katika hali ya kuvutana walinzi na kijana huyo, walijikuta nje ya ukumbi walikokuwa wamekaa wafuasi wengine, kuanzia hapo eneo hilo likageuka uwanja wa masumbwi.
Purukushani zilianza kati ya kijana mmoja na walinzi kadhaa wa mkutano huo, hatimaye haikujulikana wengine walitoka wapi, ikawa ni piga nikupige.
Ugomvi huo ulikuwa kati ya wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu dhidi ya wafuasi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Ingawa uchaguzi unaofanywa ni wa wanawake, lakini waliorushiana ngumi walikuwa wanaume.
Ugomvi ulidumu kwa takriban dakika 15, muda mchache baadaye gari aina ya Prado lililodaiwa kubeba baadhi ya watu waliokuwa sehemu ya ugomvi huo liliondoka kwa kasi kwenda uelekeo wa Manzese.
Hata hivyo, Mwananchi iliarifiwa kuwa, baadhi ya walinzi wanaodaiwa kumuunga mkono Lissu, walinyimwa vitambulisho vya kuifanya kazi hiyo, hivyo hawakutakiwa kuonekana hapo.
Baada ya ugomvi huo wa ngumi, baadhi ya waliokuwepo eneo hilo walitupiana lawama wakisema inawezekanaje waalikwe watu wa kupigana wenyewe kwa wenyewe.
“Inakuwaje mwana Chadema unaalika watu wa kumpiga mwanachadema mwenzake, wakati huu ni uchaguzi,” amesikika mmoja wa mashuhuda aliyekuwa amevalia gauni lenye nembo ya Bawacha.
Haikuchukua dakika 20, askari wa Jeshi la Polisi walifika eneo hilo, kuimarisha ulinzi na usalama, ukimya uliokuwepo usingeamini kama eneo hilo zimetoka kupigwa ngumi muda mchache uliopita.
Askari wa jeshi hilo, waliwasili katika eneo hilo, saa 7:00 usiku wakiwa kwenye gari kutokea uelekeo wa Daraja la Kijazi, Ubungo.
Baada ya polisi kuegesha gari lao, baadhi ya askari walishuka kuzunguka eneo hilo, huku wengine wakisalia ndani ya gari.
Kulikuwepo na wengine waliokwenda kwa walinzi wa mkutano huo kwa mazungumzo ya hapa na pale na baadaye mmoja alikwenda ukumbini.
Pamoja na ujio wa askari hao, kulikuwa na vijana mbalimbali waliokaa kwa vikundi vikundi nje ya ukumbi huo wakizungumza kwa taratibu.
Gari hilo liliegeshwa pembeni kidogo na ulipo ukumbi huo, askari waliendelea kuzunguka huku na kule kuimarisha ulinzi.
Uimara wa ulinzi, ulifanya watu wasio wajumbe halali wa mkutano huo, waketi umbali wa mita 100 kutoka lilipo lango la ukumbi.
Tofauti na ilivyozoeleka kushuhudiwa pilika za ingia toka za wajumbe wakati wa chaguzi kama hizo, kwa Bawacha hakukuwa na hali hiyo.
Safari pekee zilizoshuhudiwa ni zile za kwenda msalani, huku wengine wasiokuwa wajumbe walijilaza sakafuni kusubiri mchakato wa kura uendelee.
Uhakiki wajumbe ulifanyika na baadaye na pazia la uchaguzi likafunguliwa rasmi kwa kuanza na nafasi za wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka Bara na Zanzibar.
Tofauti na ilivyokuwa wakati wa uchaguzi wa Bavicha, kwa Bawacha haikuwa rahisi kupenya hata usikilize sehemu ya sera za wagombea, ulinzi ulikuwa mkali.
Licha ya kuwa uchaguzi wa Bawacha lakini, wanaume nao hawakukosekana walikuwa nje ya ukumbi wakifuatilia kwa namna moja au nyingine.
Hadi saa 11:46 alfajiri makada wa chama hicho waliokuwa wanafuatilia mkutano huo, walijilaza maeneo mbalimbali kusubiri matokeo.
Wapo waliojilaza nje ya ukumbi huo na wengine ndani ya jengo la Ubungo Plaza lakini si katika ukumbi wa mikutano.
Muda huo palianza kupambazuka na tayari uchaguzi huo umeingia siku ya pili, ukafika wakati wa wagombea wa ujumbe wa Baraza Kuu la Bawacha taifa kuanza kujinadi.