Dar es Salaam. Ukomo wa hedhi (menopause) ni kipindi cha maisha ya mwanamke kinachotokea afikiapo umri wa miaka kati ya 45 hadi 55, japo wapo wanaoweza kupata mapema au kwa kuchelewa.
Hali hii husababisha kupungua kwa uzalishaji wa homoni za oestrojeni na progesterone, jambo linalosababisha mabadiliko mengi ya kiafya na tabia.
Kisayansi oestrojeni ni homoni ya kike inayozalishwa na ovari (mayai) ambayo kazi yake kubwa ni kuhakikisha ukuaji wa viungo vya uzazi kama vile tumbo la uzazi (uterus), ovari na mrija wa fallopian na mchakato mzima wa ovulation unafanyika vizuri.
Mchango wa homoni hii, kwenye mwili wa mwanamke ni kufanya mabadiliko ya kimwili na saikolojia wakati wa mzunguko wa hedhi, ujauzito na kipindi cha ukomo wa hedhi.
Kadhalika, homoni ya progesterone, inayozalishwa ndani ya ovari, baada ovulation, ina kazi ya kudumisha mzunguko wa hedhi, kulinda ujauzito na kuufanya uwe na mazingira bora mpaka kujifungua.
Kazi nyingine, ni kuongeza kinga ya mwili kipindi cha ujauzito, kubadilisha mfumo wa matiti na kuanza kutengeneza maziwa, kupunguza nguvu za misuli ya tumbo ili kumlinda mama na kukosa choo kipindi cha ujauzito.
Wakati wa ukomo, kiwango cha oestrojeni na progesterone kinapopungua kwa kasi, wanawake wengi huanza kushuhudia mabadiliko katika mwili na hali ya kihisia kwa ujumla.
Kupungua kwa homoni hizi kunaweza kuleta madhara kadha wa kadha kwa kuwa oestrojeni na progesterone zina majukumu muhimu katika afya ya mwili wa mwanamke.
Uthibitisho mabadiliko ya kihisia
Kwa mujibu wa Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Jane Muzo, kati ya mabadiliko ya tabia anayokumbana nayo mwanamke aliyefika ukomo wa hedhi, ni pamoja na kupoteza kumbukumbu na wengine hupoteza hamu ya tendo la ndoa.
“Kutokuwa na kukosa hisia ya kufanya tendo la ndoa, hapa wengi huanza kupuuzia baadhi ya mambo, hasa kwa wanandoa, na kuwa, hali hii huwa tofauti na kipindi kingine chochote, na kuwa ana hasira na hata hushindwa kufanya vile vitu pendwa alivyokuwa akifanya awali,” anasema.
Kwa kuwa uwepo wa homoni hizi mbili huhusika na kuupa mwili usingizi, kulinda joto la mwili, kuipa ngozi, nywele na mifupa afya, kuupa mwili hisia na kumlinda mwanamke na maumivu ya mgongo, saratani ya matiti, kizazi na kulinda mfumo mzima wa moyo.
Muzo anasema wakati huo ubongo, ngozi, misuli na hisia huathiriwa kutokana na kukosekana kwa vichocheo hivyo.
Akizungumzia kuwahi au kuchelewa kwa menopause, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Abdul Mkeyenge anasema kwa mwanamke kufikia ukomo wa hedhi hutokana na kuwahi au kuchelewa kwa mwanamke huyo, kuvunja ungo.
“Wale waliowahi kuvunja ungo lazima watawahi kufikia ukomo wa hedhi na wale waliochelewa vivyo hivyo watachelewa kufikia ukomo,” anasema.
Anasema hakuna njia ya kuchelewesha kipindi hiki kwa mwanamke na kuwa, hali hiyo iko kibaoilojia zaidi na huanzia miaka 45 mpaka 55.
Mkeyenga anasema, kuna dalili mwanamke ataziona anapokaribia kufika kwenye ukomo ambazo huzifanya bila kupenda.
“Mwanamke anayekaribia hali hii hupata maudhi madogo madogo ambayo kitaalamu tunaziita menopause syndrome,” anasema.
Maudhi hayo ni pamoja na hasira za karibu kwa watoto wake, joto kali la mwili na kuwashwa mwili mzima.
“Kuna wanawake huwashwa mwili mzima mpaka kufikia kujikuna na vitu vyenye ncha kali na hata kujichuna ngozi, yote hii ni dalili za mwanamke kufikia ukomo,” anasema.
Madhara mengine ni pamoja na magonjwa kadha wa kadha kama mifupa kukosa nguvu, kukosa hamu ya tendo na mengine, anasema Mkeyenge.
Daktari bingwa wa kinamama na uzazi, Isaya Mhando anasema hakuna njia mahsusi ya mwanamke kuchelewa kuingia ukomo wa hedhi.
“Mtoto wa kike anapozaliwa anakuwa na mayai milioni mbili, anapofikia kipindi cha balehe mayai yanakuwa yameshapungua mpaka 450,000 hadi 350,000 ambayo kila mwisho wa mwezi idadi kadhaa ya mayai inakua na ndipo anapopata hedhi,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema lazima liwepo moja linalokua kwa kasi kuliko mengine, ambalo huchaguliwa kubeba mimba likikutana na mbegu inakuwa mbegu bora, na mwanamke anapofikisha umri wa miaka 35 mpaka 40 nguvu ya mayai inaanza kupungua.
“Kwenye mayai mfumo wa hedhi vile unavyoonekana mpaka ngozi inavyoonekana, nyororo na ngozi inatokana na mfumo wa homoni kutoka kwenye mayai.
“Anapozidi kuzeeka idadi ya mayai inapungua na unaanza kupata madhara joto kali, maumivu ya mgongo, kupungua kwa madini ya calcium kwenye mifupa. Kina mama wanashauriwa kuepuka vyakula vyenye mafuta yatokanayo na wanyama,” anasema.
Hata hivyo, Dk Mhando anasema hakuna uwezekano kwa mwanamke kuchelewesha ukomo wa hedhi, isipokuwa atachelewa iwapo hatavunja ungo mapema, “Bado watafiti wanalifanyia kazi hili kujua iwapo hali hii inaweza kucheleweshwa kwa mwanamke.”
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2015 walibaini kuwa wanawake wanapofikia ukomo wa hedhi wanakutana na hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo na kisukari kutokana na upungufu wa homoni ya oestrojeni na progesterone.
Ripoti nyingine ya mwaka 2016 WHO ilibaini kuwa kipindi hicho wanawake huwa hatarini kuathirika na kupooza, saratani ya matiti na kizazi na hata kupoteza kumbukumbu.
Kadhalika mwaka 2017 WHO ilifanya utafiti kuhusu afya ya akili na uzeekaji na kugundua kuwa, ukomo, husababisha mabadiliko ya homoni kwa mwanamke na kuwa na hisia mchanganyiko (mood swings), wasiwasi, huzuni na upungufu wa kumbukumbu.
Kwa mujibu wa tafiti za WHO, wanawake wanapofikia ukomo wa hedhi wanakuwa na hatari ya magonjwa ya moyo.
Kupungua kwa homoni ya oestrojen kunachangia kupoteza kinga dhidi ya magonjwa ya moyo na kiharusi, wengi waliopo kwenye hatari ya magonjwa ya moyo, hasa wale wenye historia ya kifamilia kuhusu magonjwa hayo japo wapo pia wanaopata magonjwa hayo pasipo historia za nyuma.
Kadhalika, utafiti uliofanywa na National Cancer Institute uligundua kuwa wanawake waliopitia ukomo wa hedhi wanaweza kuwa na hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti. Hii ni kutokana na mabadiliko ya homoni, ambapo upungufu wa oestrojeni baada ya menopouse unaweza kuongeza hatari ya saratani ya matiti na kwa asilimia kubwa kwa wenye tatizo la kurithi.
Saratani ya kizazi ni aina nyingine ya gonjwa ambalo linatajwa kuwapata wanawake waliofikia ukomo wa hedhi.
Tafiti nyingine maarufu kuhusu magonjwa yanayoweza kumpata mwanamke aliye kwenye ukomo ni mifupa kuwa laini na hafifu ambayo kitaalamu huitwa steoporoz. Utafiti wa American Society for Bone and Mineral Research (ASBMR) mwaka 2017 ulielezea namna upungufu wa estrogen unavyoathiri mifupa na kuleta hatari pamoja na magonjwa ya shinikizo la damu na kisukari.