Mara nyingi tumekuwa tukiona tatizo la kutopenda kula zaidi nyakati za utotoni, lakini kumbe tatizo hili linaweza kujitokeza ukubwani, chanzo kikiwa tatizo la kisaikolojia au kiakili.
Anorexia Nervosa ni ugonjwa wa akili unaosababisha muathirika kuwa na hofu kali ya kupata uzito au unene, hivyo kupoteza hamu ya kula kabisa, hatimaye kupoteza uzito mwingi unaohatarisha afya ya mwili.
Ni tatizo ambalo linawapata zaidi wasichana wa kisasa, wasomi hasa wa maeneo ya mjini ambao hupenda na kuwa na maumbile madogo ya kuvutia.
Ingawa hata wanaume wanaweza kupata, tafiti zinaonyesha kuwa tatizo hili ni maarufu zaidi kwa wasichana au wanawake kuliko wavulana au wanaume.
Hupunguza kula kwa makusudi, huku pia wakifanya mazoezi ya kupunguza uzito kuliko kawaida au hata kufanya njia nyingine za kupunguza uzito zisizo sahihi, ikiwamo vidonge vya mitaani.
Chanzo halisi cha tatizo hili bado hakifahamiki, lakini yapo mambo yanayohusishwa, ikiwamo chembe za urithi na vichocheo, jamii zinazohamasisha kujikondesha na matatizo katika familia.
Vihatarishi ni pamoja na tabia ya kupenda kuwa sahihi au kupenda kutilia mkazo kwenye mambo yasiyo na ulazima au hulka ya kutaka vitu vifanyike kwa usahihi uliokithiri.
Kwa kawaida huanza kipindi cha utotoni kwenye miaka kati ya 10 mpaka 19 au miaka ya mwanzo ya ujana, yaani miaka ya mwanzo ya ishirini.
Vilevile wanawake wenye hulka za kimagharibi, hasa walio na elimu nzuri na wenye daraja la maisha ya kati au juu na wanaotoka katika familia zenye mtindo wa maisha ya kisasa.
Mgonjwa huwa na dalili na viashiria kama vile kuwa na hofu iliyopitiliza ya kuogopa kuongezeka uzito au kuwa mnene, hata kama atakuwa amekonda, kuwa na tabia ya kutotaka kuwa na uzito unaokubalika kuwa wa kawaida kulingana na urefu na umri wake, hisia potofu kuhusu umbo lake.
Ni kawaida kwa wanawake hawa kukosa hedhi kwa kipindi cha miezi mitatu au zaidi bila hata kuwa mjamzito au kuumwa magonjwa ya kinamama.
Tabia ya kujinyima chakula kupita kiasi, wanaweza kula na kisha hukimbilia chooni kujitapisha au kunywa dawa za kujilazimisha kuharisha.
Hupenda kufanya mazoezi ya mwili kila wakati, hata kama mazingira hayaruhusu.
Kukimbilia chooni au bafuni mara baada ya kumaliza kula na pia kukwepa kula mbele ya watu wengine, hususan wageni, hupenda kutumia dawa za kuwafanya wakojoe sana, kuharisha, kutapika, kupunguza hamu ya kula na za kuondoa mafuta mwilini.
Dalili nyingine ni kuwa na ngozi kavu ya njano iliyokakamaa yenye vinyweleo dhaifu kuliko kawaida, kuchanganyikiwa, uwezo mdogo wa kufikiri, ukosefu wa kumbukumbu na udhaifu wa kufanya maamuzi.
Vilevile kuwa na msongo wa mawazo, midomo huwa mikavu, kuhisi baridi kuliko kawaida, kuvaa nguo nyingi ili kuongeza joto mwilini na mifupa yao huwa mifupi na kukonda sana.
Tatizo hili ni hatari kwa sababu linaweza kuathiri ogani za mwilini, hatimaye kifo. Habari nzuri ni kuwa ni tatizo linaloweza kutibiwa.
Fika mapema katika huduma za Afya endapo una viashiria na dalili za kutlopenda kula, inaweza kuwa ni tatizo la kiakili linalohitaji ushauri tiba kutoka kwa wataalamu wa afya ya akili.