Serikali yataja vikwazo 10 matumizi ya nishati safi, mikakati kuvikabili

Dar es Salaam. Wakati Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mwenyekiti mwenza katika mkutano wa nishati safi ya kupikia Afrika utakaofanyika nchini Ufaransa, Serikali imebainisha changamoto 10 kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi pamoja na mikakati ya namna ya kukabiliana nazo.

Mkutano huo unafanyika kesho Jumanne, Mei 14,2024 nchini Ufaransa, Rais Samia amealikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa  Nishati (IEA), Dk Fatih Birol  kutokana na kile kilichoelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba ni kutambuliwa kwa juhudi zake za kutambua umuhimu wa nishati hiyo kuweka msukumo kutokomeza nishati chafu.

Kupitia mkakati wa nishati safi, changamoto zilizotajwa ni uelewa mdogo wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, uhaba wa malighafi na miundombinu ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini, gharama kubwa ya awali na matumizi ya nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia.

Nyingine ni upungufu na ukinzani wa sera, sheria, kanuni na miongozo kuhusu nishati ya kupikia, uwekezaji mdogo katika nishati safi ya kupikia pamoja na  uwezo mdogo wa watekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia.

Pia lipo tatizo la wigo wa tafiti na ubunifu wa teknolojia zinazohusu nishati safi ya kupikia, maambukizi ya VVU na Ukimwi katika shughuli za nishati ya kupikia na uhitaji wa jitihada za kutosha za kujumuisha usawa wa jinsia katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia.

Mbali na hayo, suala la uhitaji wa kuimarisha utawala bora katika masuala yanayohusu nishati safi ya kupikia limeguswa kuwa miongoni mwa changamoto.

Hayo yameainishwa na Wizara ya Nishati kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 uliozinduliwa na Rais Samia Mei 8, 2024.

Mkakati huo ulitokana na uhitaji wa kuwa na mpango jumuishi wa kitaifa katika kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya, kiuchumi na kijamii zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.

Kuhusu suala la uelewa, mikakati itakuwa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia pia kuhamasisha wananchi na taasisi kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipiga makofi na Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Mashaka Biteko pamoja na Waziri wa Nchi, Muungano na Mazingira Dk Selemani Jafo baada ya kuzindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam Mei 68, 2024.

“Eneo la upatikanaji wa nishati safi,mkakati utakuwa ni kuboresha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uzalishaji, upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa nishati safi ya kupikia na kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia,”umeainishwa kwenye mpango huo.

Hata hivyo kuhusu gharama za nishati safi,mkakati utakuwa ni kuhakikisha gharama za awali na matumizi ya nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia zinapungua na kuhamasisha taasisi za kifedha kuwezesha wadau wa nishati safi ya kupikia.

Vilevile,upungufu na ukinzani wa sera,mkakati wake utakuwa ni kupitia, kuandaa na kufanya maboresho ya sera, sheria, kanuni na miongozo inayohusu nishati ya kupikia na kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo inayohusu nishati ya kupikia.

Ufumbuzi wa uwekezaji mdogo, kuhamasisha sekta binafsi kutumia fursa za biashara zilizopo katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia,kuhamasisha matumizi ya mifuko ya fedha na Programu za Kitaifa na kimataifa katika kukuza na kuendeleza uwekezaji katika nishati safi ya kupikia.

“Kuhusu uwezo mdogo wa watekelezaji wa miradi,mkakati ni kuwezesha upimaji wa viwango vya ubora wa nishati, vifaa na majiko ya nishati ya kupikia na kuhakikisha watekelezaji na wasimamizi wa miradi ya nishati safi ya kupikia wanajengewa uwezo,kuhakikisha ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia,” mkakati huo umebainisha.

Kwa upande mwingine wa uhaba wa tafiti, ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia katika nishati safi ya kupikia, mkakati wake ni kuimarisha uwezo wa taasisi na vituo vinavyofanya tafiti, ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia zinazohusu nishati safi ya kupikia.

Pia kuimarisha ushirikiano kati ya wawekezaji wa nishati safi ya kupikia na taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya elimu ya ufundi na ufundi stadi na vyuo vya elimu ya juu na ufundi.

Mkakati mwinginie ni usimamizi madhubuti wa rasilimali na kuzuia rushwa katika masuala yanayohusu nishati safi ya kupikia kutekelezwa ifikapo Julai, 2025,”imeandikwa kwenye mkakati huo.

Related Posts