Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetangaza kusitisha matumizi ya namba za utambulisho kwa wale waliokaidi kuchukua vitambulisho vyao.
Tangazo hilo linakuja ikiwa zimesalia siku 15 kufikia ukomo wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, la kusambaza vitambulisho milioni 1.2 vilivyotengenezwa na mamlaka hiyo, ambapo vitambulisho hivyo bado havijachukuliwa na wenyewe.
Januari 13, 2025, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Waziri Bashungwa alieleza kuwa tangu atoe agizo hilo, vitambulisho 400,000 kati ya vile vilivyokuwa vimekaa ofisini kwa muda mrefu vilitolewa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Nida leo Ijumaa, Januari 17, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo James Kaji ilieleza wale wote ambao hawajajitokeza kuchukua vitambulisho vyao na watakaopokea ujumbe mfupi wa maandishi katika simu zao, wanatakiwa kufika katika ofisi za NIDA za wilaya walizojiandikisha kuchukua vitambulisho vyao.
“Watakaoshindwa kufanya hivyo, matumizi ya namba yao ya utambulisho wa taifa (NIN) yatasitishwa baada ya mwezi mmoja tangu kupokea ujumbe huo,” imeeleza barua hiyo.
Agizo hilo linatolewa baada ya mamlaka hiyo kugundua kuwa licha ya kupeleka vitambulisho katika kata, vijiji, mitaa, vitongoji na shehia ili kuwaridhisha wananchi, bado wananchi wengi hawajajitokeza kuvichukua.
NIDA imefanya kazi ya uzalishaji na usambazaji wa vitambulisho vya taifa kwa umma tangu Oktoba 12, 2023, na linatarajiwa kumalizika Machi, 2024. Tangu kuanza kwa kazi hiyo, vitambulisho vimepelekwa katika ofisi za watendaji wa kata, vijiji, mitaa, vitongoji na shehia, na wananchi waliombwa kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao. Hata hivyo, mpaka sasa, vitambulisho vingi bado havijachukuliwa.
Ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho, NIDA imeanzisha mfumo mpya wa kutuma ujumbe mfupi wa simu kwa wananchi wanaohitaji kuchukua vitambulisho vyao, ili kuhakikisha kila mtu anapata kitambulisho chake. Hadi sasa, ndani ya siku mbili, NIDA imewafikia watu 400,000 katika wilaya 87 kati ya wilaya 153.
NIDA inasema kuwa ifikapo Januari 31, 2025, itakuwa imesambaza vitambulisho vyote kama ilivyoagizwa.