Mbowe kuja na mapendekezo mapya ya uongozi Chadema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema iwapo atafanikiwa kushinda uongozi wa juu wa chama hicho, atapeleka mapendekezo kwenye mkutano mkuu ili uchaguzi wa ndani uwe unafanyika kila baada ya miaka mitatu badala ya mitano.

Mbowe, anayetetea nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21, amesema hatua hiyo itakifanya chama hicho kujiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na miaka miwili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ili kuepuka kinachotokea sasa.

Mbowe amesema hayo na mengine mengi katika mahojiano yake na wahariri na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) leo Ijumaa, Januari 17, 2025, kuelekea uchaguzi wa Chadema utakaofanyika Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Mbowe anashindana na wagombea wenzake watatu, Charles Odero na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Tundu Lissu. Hali hiyo imeibua minyukano ndani na nje ya chama.

Mbowe amesema iwapo atashinda tena, atapeleka pendekezo kwa mkutano mkuu kuwa uongozi uwe unakaa miaka mitatu ili kutoa chama nafasi ya kujiandaa kwa chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

“Ikiwa uongozi wa sasa utaingia mwaka 2025, ina maana Januari 2028 mpaka Desemba tuanze mwaka wa uchaguzi ndani ya chama ili 2029 tuwe na uongozi mpya ndani ya chama.

Mwenyekiti wa Chadema na mgombea wa nafasi hiyo, Freeman Mbowe (katikati), akizungumza wakati akifanya mahojiano na wahariri na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd yaliyofanyika makao makuu ya MCL jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, Januari 17, 2025.

“Uongozi uwe na mwaka mmoja kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na miaka miwili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ili kuondoka katika hili ambalo limetokea,” amesema Mbowe.

Kuunda tume ya ukweli na upatanishi

Mbowe amesema iwapo atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, ataunda tume ya ukweli na upatanishi.

Amesema katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho kuanzia ngazi za chini hadi wa taifa, utakaohitimishwa Jumanne ya Januari 21, 2025, kumetokea mnyukano mwingi unaohitaji kupata mapatano.

“Tukimaliza uchaguzi, tutafuata utaratibu unaofanyika duniani kote kutengeneza mapatano na kutibu majeraha ya uchaguzi.

“Kutengeneza tume ya ukweli na upatanishi kwa sababu watu wamekanyagana sana. Watu wameumizana sana. Nikichaguliwa, tutaitana na kuzungumza kwani tunahitajiana wote,” amesema Mbowe.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali

Related Posts