WANA CCM YAPO YA KUJIFUNZA KWA ABDULRAHMAN KINANA

Na Said Mwishehe 

NGOJA nikwambie kitu mtu wangu ingawa najua itakuwa unafahamu kwamba Chama Cha Mapinduzi(CCM) Januari 18 hadi 19 mwaka huu wa 2025 kinafanya mkutano mkuu maalum.

Tufanye hivi ajenda zinaweza kuwa zaidi ya mbili au tatu lakini unachotakiwa katika akili yako ni ajenda kuu ya mkutano huo ni kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Abdulrahman Kinana kuomba kupumzika,hivyo amekuwa kando kwa muda sasa. 

Kama unakumbuka au nikukumbushe tu Mzee Kinana aliandika barua kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na alijibiwa ombi lake kwa kukubaliwa na Dk.Samia. 

 Hivyo wana CCM Januari 18 hadi 19 wanakuta katika Jiji la Dodoma ambako ndipo yalipo makao makuu ya Chama hicho kuchagua Makamu Mwenyekiti.Swali kuu linabakia kuwa nani atakuwa mrithi wa Kinana? 

Swali hili zimebakia saa chache tutafahamu.Vuta subira kwani subira inaleta heri. Lakini ngoja nizungumze kidogo kuhusu Kinana ambaye ni mwanasiasa mkongwe,maarufu  na aliyejijengea heshima kubwa ndani ya Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa ujumla.

Kinana ana sifa ya ziada maana sio mwanasiasa tu bali ni kiongozi. Uwezo wake katika kuamua mambo,kusuka mikakati pamoja na kusimamia malengo umemfanya awe mwanasiasa aliyejitofautisha na wanasiasa wengi ndani ya nchi yetu.

Kwa wanaomfahamu Kinana wanielewa vizuri.Ametengeneza sayari yake katika siasa za Tanzania. Kwa faida yako msomaji unayesoma makala hii ni kwamba Kinana kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM mwaka 2012 alishakuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya  Chama hicho kwa zaidi ya miaka 30, sasa hapo ongeza ni miaka yake akiwa Katibu Mkuu wa CCM na baadae Makamu Mwenyekiti. Kwa lugha rahisi kabisa ni kwamba Kinana amekuwa katika Chama Cha Mapinduzi kwa zaidi ya miaka 40.

Huyo ndiye Kinana ambaye nafasi yake inakwenda kujazwa katika siku hizo. Nikurudishe nyuma tena kidogo baada ya Kinana kuona amekitumikia chama hicho kwa miaka 30 aliomba kupumzika ili kutoa nafasi kwa vijana kuendelea pale alipoishia.

Ombi lake la kutaka kustaafu siasa mwaka 2012 liligonga mwamba, Wana CCM kwa kutambua uwezo na mchango wake walimuomba abakie ndani ya chama hicho. Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa wakati ule alikuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete maarufu Mzee Msoga hakuwa tayari na uamuzi wa Kinana hivyo kupitia Kamati Kuu akamteua kuwa Katibu Mkuu. 

Ngoja nikwambie kitu msela wangu Kinana alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu hapo wasiojua kwanini Kikwete na CCM walimng’ang’ania abakie. Iko hivi katika historia ya Chama hicho Kinana anaingia katika orodha ya Makatibu Wakuu waliowahi kukitumia chama kwa utendaji uliotukuka.

Kwangu namhesabu Kinana kama Katibu Mkuu namba moja kiutendaji.Ninazo sababu za kuthibitisha hilo,nitataja chache. Kinana akiwa Katibu Mkuu katika nafasi ya Msemaji wa Chama alikuwa Nape Nnauye.

Kinana peke yake kama katika soka basi unaweza kumfananisha na Christiano Ronaldo au Messi lakini ukitaka kueleza vizuri waunganishe kwa Pamoja wachezaji hao kupata uwezo wao katika mpira lakini wewe mfano huo uwe katika medani ya siasa.

Huyo ndio Kinana Lakini hoja yangu yangu kubwa ninapomzungumzia Kinana ni mwanasiasa mwenye kujua kuzungumza kwenye meza ya majadiliano na hii ni moja ya sifa yake ya pekee katika kuandaa mikakati au “strategies.” 

Akiwa Katibu Mkuu Kinana kupitia uwezo mkubwa wa kisiasa na kiungozi baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo aliamua kufanya ziara ya kuzunguka katika majimbo yote uchaguzi, Wilaya zote, Halmashauri zote pamoja na mikoa yote nchini. Kinana alipita karibia nusu ya vijiji vya Nchi yetu.

Binafsi nashukuru Mungu nilibahatika kuwamo katika ziara zake zilizoanza mwaka 2012 hadi mwaka 2015. Asikwambie mtu Kinana ameacha alama ndani ya CCM. 

Alipita katika milima,mabonde,katika vumbi, katika lami,alivuka mito ,maziwa na bahari akienda kukijenga Chama hicho tena katika nyakati ambazo mwana CCM akivaa sare ya ccm anazomewa mtaani. 

CCM ilikuwa katika wakati mgumu sana wakati ule .Huku mtaani watu walikuwa na People Powers a.k.a CHADEMA tena CHADEMA ya moto kweli kweli sio Chadema hii ya sasa nusu iko duniani,nusu inachungulia kaburi. 

Basi Kinana akawa na kazi ya kufufua uhai wa Chama chake, haikuwa kazi rahisi ,alijenga hoja kueleza mazuri ya CCM na kisha akaamua kuitenganisha CCM na madudu yaliyokuwa yanafanywa na Serikali.

Unakumbuka kauli ya Mawaziri Mizigo? Kazi ya Kinana ya kurejesha matumaini ya CCM kwa Watanzania ilikuwa ngumu lakini aliishinda na hatimaye CCM ikarejea katika mstari, waliokuwa wanamfuatilia wakati ule wanajua ninachozungumza.

Kwa kifupi Kinana alipokuwa Katibu Mkuu alitumia akili na maarifa yake kuhakikisha mambo yanakuwa shwari. Misaada ya hali na mali aliyoitoa kwa wananchi alipokuwa Katibu Mkuu itabakia katika vichwa ya Watanzania kwa muda mrefu.

Hakuwa na ubaguzi alihakikisha anatafuta ufumbuzi wa changamoto za watu. Hata shida binafsi alizipatia majibu hasa zilizokuwa ndani ya uwezo wake.

Ukiniuliza Katibu Mkuu gani amefanya aliyoyafanya Kinana, jibu hakuna. Na hapa Naomba nieleweke siwashindanishi lakini najaribu kutoa maoni yangu,nawe ukitoa ya kwako nitasoma. 

Kinana huyu ambaye nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti inakwenda kupata mrithi wake katika siku mbili naamini anapumzika katika siasa lakini kuna wana CCM watakuwa wanasema kimoyo moyo kwanini ameamua kukaa pembeni? Si angeendelea tu ? Lakini ukweli kwa muda ambao amekitumikia Chama hicho acha akapumzike. 

 Kinana katika uongozi wake haamini katika kukaa ofisini, anaamini katika kwenda saiti, sio kiongozi wa kukaa katika kiti na kutoa maagizo. Ni kiongozi ambaye anataka kusikiliza changamoto za wananchi kwa kuwafuata katika maeneo yao. Hii imemfanya kujijengea heshima yake,anakubalika na anapendwa ukiuliza sababu utaambiwa ni mwanasiasa aliyeamini katika utu na ubinadamu.

Kinana sio wale viongozi wapandisha mabega na kujikweza. Katika maisha yake anaamini katika kujishusha lakini sifa yake nyingine tena kubwa hayuko tayari kuona heshima na jina lake linachafuliwa kirahisi.Haamini katika siasa za visa na hila.

Kinana ni mwanasiasa anayeamini katika siasa za hoja sio siasa za vihoja. Ni Kinana huyu akiwa Makamu Mwenyekiti alienda na staili yake ya kwenda kuzungumza na wana CCM katika maeneo yao.Akiwa Makamu Mwenyekiti amesikiliza na kutatua changamoto nyingi kwa maelekezo ya Chama chake.Hivyo Kinana anapumzika siasa anaacha alama katika kila nafasi aliyoitumikia ndani ya Chama hicho. 

 Hebu tuulizane nani hajui kazi ya Kinana aliokuwa Meneja Kampeni wa Rais mstaafu Hayati Benjamin Mkapa mwaka 1995? Kinana kwa uwezo wake wa kupanga mipango ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu alikuwa Meneja Kampeni pia hata kwa Rais Mstaafu Kikwete na kwa Hayati Rais Dk.John Magufuli. Akiwa Meneja Kampeni amefanikiwa kukiwezesha Chama hicho na wagombea wake kushinda kwa kishindo.

Kwa kuwa nimemua kumueleza Kinana ndani ya CCM sitagusia alipokuwa Waziri wa Ulinzi,sitazungumzia akiwa jeshini.Namzungumzia Kinana wa CCM. Hata hivyo wakati akiamua kupumzika katika medani za kisiasa amekuwa mwalimu kwa wanasiasa wengi hasa vijana wenye ndoto za kuwa wanasiasa wakubwa.

Kupitia matendo, kauli, jinsi anavyoshughulikia mambo na anavyoishi na watu ni darasa tosha kwa wanasiasa wanaotaka kujifunza siasa na uongozi. Kinana amejaaliwa utu sana na hili ni darasa jingine kwa wanasiasa hasa wa CCM.

Amekuwa ni kiongozi wa kujitoa na kusaidia wengine. Kwasasa kuna wanasiasa wengi wale wa nipe nikupe,tunao wanasiasa wanaoamini cheo ndio kila kitu,asiye nacho basi ni kama takataka. Kwa Kinana ni tofauti na cheo kwake ni utumishi sio utukufu. 

Tunao wanasiasa wengi wanavimbisha mabega utadhani kobe anakwepa mwamba chini ya bahari, tunao wanasiasa wanaojiona wao ndio kila kitu.Sio kwa Kinana kwani na nguvu aliyonayo katika siasa amebakia kuwa mtu mwadilifu na mwaminifu,amebakia kuwa Kinana anayeamini cheo kinapita. 

 Wana CCM naomba mjifunze kupitia Kinana hasa wanasiasa vijana, Kinana hayuko katika kundi la wanasiasa jeuri na viburi.Kinana anastaafu siasa akiwa mwanasiasa anayeamini katika utu. 

Kwangu yapo niliyojifunza kutoka kwa Kinana nanikiri mafunzo yake yamenisaidia sana katika kuishi na watu iwe katika kazi au mtaani.Wana CCM narudia tena yapo ya kujifunza kutoka kwa Kinana.Najua naye ni binadamu sio malaika, lakini kuna mengi ya kujifunza kwake,amejaaliwa hekima,amejaliwa busara. 

Alamsiki,tuelekezo macho na masikio Dodoma Januari 18 na 19 mwaka huu.Wajumbe wa Mkutano Maalum kila lenye heri likawe kwenu,mnaye Mwenyekiti na Rais mahiri sana .CHAMA CHENU WANA CCM CHINI YA DK.SAMIA MKO SALAMA SANA.NA MKUMBUKE MWAKA HUU NI WATANZANIA NA SAMIA TU.  

Mawasiliano yangu 0713833822/0762451570.

Related Posts