Tanimu: Singida Black Stars imepata jembe

BEKI wa kati wa zamani wa Singida Black Stars anayeichezea Crawley Town ya Uingereza, Benjamin Tanimu amempongeza Mnigeria mwenzake, Amas Obasogie kujiunga na Singida Black Stars kutoka Fasil Kenema ya Ethiopia, huku akisema kwa timu aliyotua imelamba dume.

Tanimu ambaye anajivunia ufanisi wake akiwa na timu hiyo kabla ya kutimka nchini, ameonyesha kuwa na imani na Obasogie akisema kipa huyo anaweza kufanikiwa zaidi katika Ligi Kuu Bara endapo ataendelea kuonyesha juhudi na nidhamu aliyokuwa nayo akiwa Ethiopia, ambako hakuruhusu bao katika michezo mitatu kati ya 11 aliyocheza msimu huu.

“Ni mchezaji mzuri na mwenye uwezo mkubwa, kwa hiyo naamini atafanya vizuri Tanzania, ingawa kikubwa ni kuendelea kujituma kama alivyokuwa akifanya huko Ethiopia,” alisema.

Kwa upande mwingine, Singida Black Stars imeendelea kujiimarisha msimu huu, ambapo maboresho makubwa yamefanywa katika maeneo ya ulinzi na ushambuliaji.

Hii inamaanisha kuwa Obasogie, ambaye ni kipa, atakutana na changamoto kubwa ya kupigania namba kwenye kikosi cha kocha Hamdi Miloud, hasa dhidi ya Metacha Mnata, ambaye amekuwa kipa namba moja wa timu hiyo msimu huu. Metacha amekuwa na kiwango cha juu, akihakikisha kuwa nyavu zake hazijaguswa katika michezo saba.

Viongozi wa Singida Black Stars wamefanya maamuzi haya baada ya kugundua kuwa Metacha hakupata ushindani wa kutosha kutoka kwa Mohamed Camara, ambaye amepelekwa kwa mkopo katika timu ya Pamba Jiji, hivyo kumwacha Obasogie na kazi kubwa ya kuthibitisha uwezo wake.

Mbali na Obasogie, Singida BS imeongeza mastaa wengine kwenye dirisha la usajili la Januari, akiwemo Serge Pokou kutoka Ivory Coast, ambaye alikuwa akichezea Al Hilal ya Sudan, na mshambuliaji wa kati Jonathan Sowah kutoka Ghana. Wachezaji hawa wametambulishwa tayari.

Kimahesabu, idadi ya wachezaji wa kigeni katika Singida Black Stars imepita idadi ya 12, ikiwa ni pamoja na wale waliorejeshwa kwa mkopo na wachezaji wapya waliotambulishwa.

Ofisa habari wa timu hiyo, Hussein Masanza alieleza kuwa taarifa kamili kuhusu wachezaji wa kigeni na wale waliotolewa itatolewa hivi karibuni, hivyo mashabiki na wadau wa soka wanatarajia kupata taarifa rasmi juu ya wachezaji hao katika kipindi hiki cha Januari.

Related Posts