WAKATI usajili wa Abdi Banda kutoka Sauzi kutimkia Dodoma Jiji ukiendelea kuwa gumzo, beki huyo mzawa ameeleza sababu za kurejea nyumbani.
Banda aliyewahi kuichezea Simba akitokea Coastal Union, kisha kutimkia Baroka FC ya Sauzi na kukipiga Mtibwa Sugar kabla ya kusajiliwa Dodoma akipewa mkataba wa miezi sita, alikuwa Baroka aliyoirudia baada ya kuzunguka klabu kadhaa nchini humo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Banda alisema Tanzania ni nyumbani hawezi kupakimbia, lakini kibali cha kufanyia kazi Sauzi kilisumbua na kitachukua muda mrefu kutoka.
Alisema aliona sio vyema kukaa tu na kuchukua mshahara bila kucheza wakati kazi yake ni kucheza ndio maana akavunja mkataba ili atafute sehemu atakayokuwa anacheza.
“Hii miezi sita sio rahisi kukaa tu bila kucheza na kama unavyojua sehemu rahisi ya kupata muda wa kucheza ni nyumbani, na ndio maana nimefanya uamuzi wa kusajili Dodoma,” alisema Banda.
“Licha ya ushindani kuwa mkubwa na mpira unazidi kupiga hatua na ndio maana nikatumia nafasi hii kutua Dodoma na kujiweka fiti kwa miezi sita kuliko nikae nisubiri dirisha kubwa.”
Mchezaji huyo aliongeza kwamba, “nikikaa tu maana yake nitakuwa sijacheza msimu mzima, Lakini si tunasema ligi yetu imekuwa kubwa basi tusishangae na wachezaji wakubwa wakirudi kucheza, maana ligi bora inachezwa na wachezaji bora.
“Kwa sasa nataka kuzingatia kuitumikia Dodoma kwa mengine tutajua baadae na nitarejea kujiunga Jumapili ili kuungana na wenzangu kambini.”