Siha yaandikisha wanafunzi 5,483 darasa la awali na la kwanza

Siha. Mkuu wa Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Dk Christopher Timbuka amesema mpaka Januari 15, mwaka huu jumla ya wanafunzi 2,819 kati ya 3,323 wameandikishwa darasa la kwanza wilayani humo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Januari 17, 2025, Dk Timbuka amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wanafunzi wote walioandikishwa darasa la awali, la kwanza na kidato cha kwanza wanasoma katika mazingira rafiki na kwamba hakuna mwanafunzi atakayeshindwa kuendelea na masomo kwa kukosa madarasa.

Amesema kwa kipindi cha mwaka 2024/25, Serikali imetoa zaidi ya Sh24 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miundombinu ya madarasa.

“Naishukuru Serikali kwa namna ilivyojenga shule katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu na kuwasogezea wanafunzi huduma karibu,” amesema Dk Timbuka.

Amesema kwa wilaya hiyo hakuna mwanafunzi anayetembea zaidi ya kilomita saba kwenda shuleni kwa kuwa vijiji vyote vina shule za msingi, na hii ni azma ya Serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma karibu na wanakotoka.

“Kwa wilaya yangu mpaka sasa wanafunzi wa darasa la kwanza ambao tumewaandikisha na wameripoti kwa hizi siku tatu ni wanafunzi 2,819 kati ya 3,323 ambao ni mategemeo yetu. Kwa hizi siku chache ambazo zimebaki katika wiki hii naamini wote watakuwa wameripoti,” amesema Dk Timbuka.

Amesema kwa darasa la awali, mpaka sasa wilaya hiyo imeandikisha wanafunzi 2,664 kati ya wanafunzi 2,975 ya matarajio yao na kusema siku zilizobaki watakuwa wamefikia matarajio yao.

“Wilaya nzima tulitegemea kuandikisha wanafunzi 2,975. Waliandikishwa kwa hizi siku tatu ni 2,664, kwa hiyo tupo vizuri kwa kuwa bado ni wiki ya kwanza na leo ni siku ya tatu,” amesema Dk Timbuka.

Amesema Serikali imeboresha miundombinu ya shule wilayani humo, ikiwemo madarasa, na kwamba mpaka sasa wako vizuri na hakuna mwanafunzi atakayeshindwa kuendelea na masomo kwa kukosa madarasa.

“Mpaka sasa tuna madarasa 64 ambayo hayajaanza kutumika. Haya yote yanasubiri wanafunzi ambao watazidi katika maeneo yetu. Lakini kwa sasa tuna wanafunzi wa kike 1,525 na wa kiume 1,675 wa kidato cha kwanza, na mpaka sasa hakuna mwanafunzi aliyekosa nafasi,” amesema Dk Timbuka.

Amesema mpaka sasa lengo la uandikishaji wa wanafunzi limetimia kwa asilimia 89 na kwamba asilimia 11 zilizosalia watawatafuta wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni.

“Hapa kwetu tuna wanafunzi wanaotokana na jamii ya kifugaji. Wapo wanaotumia watoto hawa katika shughuli za kifugaji na wanafanya hivyo wakati wa likizo. Wapo wanaoishi na bibi zao, lakini hawa wote tunawafuatilia kuhakikisha wanarudi shuleni,” amesema Dk Timbuka.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa huo, Kisseo Nzowa amesema Serikali mkoani humo imeweka mazingira mazuri na wezeshi ya ufundishaji kwa wanafunzi wote.

“Mwitiko kwa baadhi ya shule umekuwa mzuri na shule zetu zote zipo tayari kuwapokea wanafunzi. Ni imani yetu kuwa kazi hii inakwenda vizuri na idadi kubwa ya wanafunzi wameendelea kujitokeza na wanaripoti wote darasani,” amesema Nzowa.

Related Posts