Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inatarajia kuandikisha wapigakura wapya 78,922 waliotimiza umri wa miaka 18 kwa mujibu wa takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika uandikishaji wapigakura awamu ya pili kwa mwaka huu wa 2025.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji George Kazi ametoa kauli hiyo leo Januari 17, 2025 alipofungua mkutano wa wadau wa uandikishaji wapigakura wapya awamu ya pili kwa mwaka 2025 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, Pemba.
Shughuli hiyo inatarajiwa kuanza Februari Mosi katika Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba na kumalizikia Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini na Magharibi Machi, 2025.
“Uandikishaji huo ni matayarisho ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 pia ni wa mwisho kuelekea uchaguzi huo,” amesema.
Akizungumzia lengo la mkutano huo amesema ZEC ina utaratibu wa kukutana na wadau kila linapotokea jambo muhimu ambalo linahitaji kuwashirikisha.
Amesema tume kupitia mikutano hiyo pia inasikiliza maoni, hoja na mapendekezo yatakoyosaidia kuendesha shughuli hiyo kwa ufanisi.
Amesisitiza kwamba, uandikishaji utawahusu wapigakura wapya ambao hawajaandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
Kazi hiyo amesema itafanyika kwa muda wa siku tatu kwa kila wilaya na kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Tume.
Amewataka wananchi waliotimiza sifa kujitokeza kutumia haki yao waweze kushiriki uchaguzi mkuu na kuwakumbusha huduma za uendelezaji wa daftari zinaendelea katika ofisi za Tume ya Uchaguzi za wilaya muda na saa zote za kazi.
Hata hivyo, amewataka wananchi na wadau wa uchaguzi Zanzibar kudumisha amani katika kipindi chote cha uandikishaji kama walivyofanikisha katika Kisiwa cha Pemba.
Amesema matumaini yake ni kwamba, wataendelea kushirikiana.
Awali, akiwasilisha taarifa na utaratibu wa uandikishaji wapigakura wapya na uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Thabit Idarous Faina, amesema wanatarajia kuweka wazi orodha ya wapigakura waliopoteza sifa na wanaohamisha taarifa zao kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 19 na 31 cha Sheria ya uchaguzi na 4 ya mwaka 2018.
Hatua hiyo amesema itaenda sambamba na uwekaji wazi orodha ya wapigakura walioandikishwa katika uandikishaji wa awamu ya pili.
Amesema ZEC inaendelea kutoa huduma ya ujumbe mfupi wa maneno (sms) ambao wapigakura wanaweza kujua taarifa zao kwa kutumia simu ya mkononi kwa mitandao yote iliyosajiliwa Tanzania na huduma hiyo ni bure haina makato.
Amewaomba wananchi na wadau wa uchaguzi kwa ngazi tofauti kushirikiana na Tume kufikisha ujumbe huo ili kuwahamasisha wenye sifa za kujiandikisha kufika vituoni wakiwa na kitambulisho cha Mzanzibari mkazi.
“Kila mwananchi ana wajibu wa kwenda kituoni kuangalia jina lake, kuona jina la mtu ambaye hahusiki kuwemo kwenye daftari hilo, ama kwa kufariki dunia au kwa namna nyingine yoyote,” amesema.
Maulid Ame Mohammed, Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Sheria akiwasilisha mada ya nafasi ya sheria katika uandikishwaji na uendelezaji wa daftari la wapigakura amesema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kila Mzanzibari aliyetimiza miaka 18 ana haki ya kujiandikisha na kupiga kura katika uchaguzi unaofanyika Zanzibar.
Akifunga mkutano huo wa wadau, Kamishna wa Tume hiyo, Awadh Ali Said amewataka wadau kutambua majukumu yao na kuwa wa kweli katika changamoto zinazojitokeza wakati wa uandikishaji ili kazi hiyo ifanyike kwa ufanisi bila ya uvunjifu wa amani.
Mratibu kutoka Umoja wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), Juma Kombo Hijja amevishauri vyama vya siasa kuwahamasisha wapigakura kwa kauli za kistaarabu na siyo kutoa kauli ambazo zinaviashiria vya uvunjifu wa amani kwani viashiria hivyo vitasababisha kundi la watu wenye ulemavu kutojitokeza na kushiriki kikamilifu.
Mkutano huo wa siku moja, umeshirikisha wadau wa uchaguzi, zikiwemo taasisi za Serikali na binafsi, vyama vya siasa, makundi maalumu, vyombo vya ulinzi na usalama na vya habari.