Polisi: Matukio ya mauaji yameongezeka, udhalilishaji ukipungua

Unguja. Wakati makosa ya udhalilishaji na ulawiti yakielezwa kupungua Zanzibar kwa Januari hadi Desemba, 2024 kwa asilimia 12.8, ya mauaji yameongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Zuberi Chembela amesema makosa 164 dhidi ya binadamu, hususani ya kubaka na kulawiti yamepuungua.

Kwa mujibu wa takwimu alizotoa Chembela, Januari hadi Desemba 2024, yameripotiwa makosa 1,116  katika vituo vya polisi Zanzibar ikilinganishwa na makosa 1,280 ya kipindi kama hicho mwaka 2023 sawa na upungufu wa makosa 164.

Ametoa takwimu hizo leo Januari 17, 2025 akitoa tathimini ya hali ya usalama Zanzibar kwa kipindi cha miezi 12.

Amesema makosa 829 ya kubaka yameripotiwa ikilinganishwa na 927 kipindi kama hicho mwaka 2023, yakiwa ni pungufu kwa makosa 98 sawa na asilimia 10.6.

“Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, jumla ya makosa 217 ya kulawiti yameripotiwa ikilinganishwa na makosa 309 ya kipindi kama hicho mwaka 2023 ni upungufu wa makosa 92 sawa na asilimia 29.8,” amesema.

Hata hivyo, amesema makosa dhidi ya binadamu yakiwamo ya mauaji yameongezeka. Ameeleza Januari hadi Desemba 2024 makosa 66 yameripotiwa ikilinganishwa na 44 ya mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la makosa 22. Amesema baadhi ya makosa yanatokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi.

Amewataka makamanda wa mikoa na maofisa wa polisi kuongeza nguvu kuzuia makosa ya mauaji, wizi wa pikipiki, wizi wa mifugo, makosa dhidi ya watalii na ya usalama barabarani ambayo yameongezeka mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Amewahimiza kushirikiana na jamii, vikosi vya ulinzi na usalama na taasisi za haki jinai katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katika matukio hayo, baadhi ni ya watu wanaodaiwa kutekwa na kukutwa wameuawa, miili kuokotwa barabarani ikiwa imeharibika na ugomvi wa wanandoa.

Ali Bakari Ali, aliyekuwa Katibu wa Chama cha ACT-Wazalendo jimbo la Chaani Mkoa wa Kaskazini Machi 2024 alipoteza maisha akipatiwa matibabu Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kukutwa akiwa ametelekezwa.

Mwingine ni Ramadhani Iddi Shaaban (48), mkazi wa Chumbuni aliyechukuliwa na watu waliojitambulisha ni askari wa vikosi vya SMZ wakidai wanampeleka Kituo cha Polisi Mwanakwerekwe kwa ajili ya mahojiano kisha mwili wake kuokotwa siku inayofuata.

Tukio lingine lilitokea Kisakasaka Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, mwili wa Kambalagula Mabula Chungwa (45), mkazi wa Fuoni Kibondeni ulipatikana ukiwa umetelekezwa pembezoni mwa barabara huku ukiwa na majeraha yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Katika tukio lingine la Septemba 20, 2024 Idarous Masoud Omar (23), mkazi wa Tomondo aliuawa saa 11:00 alfajiri maeneo ya Mombasa Wilaya ya Magharibi B akituhumiwa kwa wizi wa pikipiki.

Oktoba 2, 2024 Masaka Juma Masaka maarufu Zahoro (40) mkazi wa Kijichi Nguruweni alimshambulia mkewe Zaituni Elias Kahindi kwa kumpiga na mchi kichwani na kusabaisha kifo chake, chanzo cha tukio ni ugomvi miongoni mwa wanandoa hao.

Mashaka alidaiwa kujinyonga Oktoba 3, 2024 kwa kutumia kamba aliyofunga kwenye mti wa mfenesi.

Askari wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ), Haji Machano Mohamed, mwili wake uliokotwa Septemba kwenye msitu ukiwa umeharibika kiasi cha kutotambulika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Daniel Shillah Septemba 28, askari huyo alipotea Agosti 8, 2024 wakati alipokuwa na wenzake katika mafunzo ya uongozi katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Dunga.

Novemba 9, 2024 watu wawili walipoteza maisha wakidaiwa kupigwa risasa na polisi kwa kosa la kukutwa na mchanga huku wanafunzi wawili Shule ya Msingi Kidoti wakijeruhiwa.

Waliofariki katika tukio hilo ni Msina Sharif (39) na msaidizi wake Abdala Bakari (28), huku waliojeruhiwa ni Mohamed Issa (10) na Hamza Abdalla Abasi (10).

Related Posts