MASHABIKI wa Yanga tangu juzi wamekuwa na presha kutokana na kutoonekana mazoezini kwa kiungo mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Pacome Zouzoua wakati zikibakia saa chache kabla ya kuvaana na MC Alger ya Algeria, lakini nyota huyo ameibuka na kumaliza utata utata huku akitoa kauli ya kibabe.
Yanga inajiandaa kushuka uwanjani jioni ya leo Jumamosi kuvaana na MC Alger katika mechi ya mwisho ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili itinge robo fainali kuungana na Al Hilal ya Sudan iliyotangulia mapema katika kundi hilo lenye TP Mazembe vilevile.
Matokeo ya sare kwa Yanga mbele ya timu hiyo ya Algeria, itakuwa na maana kwamba watetezi hao wa Ligi Kuu Bara itaaga michuano, kwa vile ina pointi saba kwa sasa wakati wapinzani wao wakiwa na nane na hivyo sare ityawabeba kuungana na Al Hilal yenye pointi 10 na itakayokuwa wageni wa Mazembe.
Hata hivyo, wakati wa maandalizi ya mchezo huo utakaopigwa kuanzia Saa 10:00 jioni kama ule wa Mazembe na Al Hilal utakaopigwa kule Lubumbashi, DR Congo, Pacome hakuonekana mazoezini na kusababisha presha kwa mashabiki, lakini nyota huyo amejitokeza na kueleza kilichomfanya akosekane.
Pacome ambaye ni miongoni mwa viungo muhimu katika kikosi cha Yanga huu ni msimu wake wa pili Yanga, huku akishiriki mechi zote za kimataifa hatua ya makundi msimu huu.
Muivory Coast huyo amecheza jumla ya dakika 443 katika mechi tano za hatua Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, hakuonekana tangu juzi mazoezini kabla ya mapema leo kuweka bayana kwamba alikuwa anaugua ndio maana alikosekana na kwamba mashabiki wasiwe na presha kwani anaamini Yanga inatoboa robo.
Pacome alisema, kwa siku mbili zilizopita alianza kuhisi hali ya tofauti kidogo kama dalili za malaria, lakini hakuacha kufanya mazoezi licha ya kuwa hakuonekana na kikosi.
“Nilikuwa nafanya mazoezi gym baada ya kupata dalili za malaria, lakini nimeomba kucheza mechi ya Leo ili nisaidie timu yangu,” alisema Pacome aliyefunga mabao matano na kuasisti tano katika Ligi Kuu Bara na kuongeza;
“Japo nimeomba ila uamuzi utakuwa kwa kocha Ramovic (Sead) kama ataona niko fiti na mchezo wa leo unanihitaji basi mashabiki wataniona.”
Wakati Pacome akiiomba mechi ya MC Alger, taarifa nyingine zinasema kuwa kiungo mshambuliaji mwingine nyota wa timu hiyo, Clatous Chama aliyerejea kutoka majeruhi yupo fifte fifte kuanza mchezo wa leo kwa kilichoelezwa bado hajaimarika kiafya licha ya kujifua na wenzake tangu kabla ya mechi iliyopita dhidi ya Al Hilal alipoingizwa dakika za lala salama kule Mauritania.
Kiungo huyo aliyepata majeraha katika mchezo dhidi ya TP Mazembe zilipocheza mara ya kwanza katika mechi za kundi hilo uliopigwa DR Congo na kumalizika kwa sare ya 1-1 na kurejea dhidi ya Al Hilal zilipovaaa Mauritania na Yanga kushinda bao 1-0 huku Chama akiingia dakika za majeruhi kumpokea Pacome, bado anaendelea kuimarika huku mchezo uliopita dhidi ya Al Hilal akianzia benchi.