Sasa kunachangamka! Mzize dau limepanda

YANGA inashuka uwanjani jioni ya leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kukabiliana na MC Alger ya Algeria katika mechi ya mwisho ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku thamani ya mshambuliaji wa timu hiyo, Clement Mzize ikizidi kupanda.

Mzize anayeongoza kwa mabao kwa Yanga katika msimu huu hadi sasa, inadaiwa amekuwa akivitoa mate vigogo vya soka Afrika ambayo zimekuwa vikituma ofa kwa mabosi wa klabu hiyo ya Jangwani ili kumnasa bila mafanikio.

Nyota huyo amekuwa na kiwango bora tangu atue Yanga ikiwa chini ya Kocha Nasreedine Nabi, kisha kunolewa na Miguel Gamondi na sasa akiwa na Sead Ramovic, kutokana na mchango wake uwanjani akishirikiana na wachezaji wenzake.

Inadaiwa kwamba hadi sasa wakati dirisha dogo la usajili la Tanzania likiwa limefungwa, kuna ofa tatu za maana zimetua mezani kwa Yanga ikiwamo ya Wydad Casablanca ya Morocco iliyokuwa tayari kutoa Dola 1 milioni moja (zaidi ya Sh 2 bilioni), huku Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na USM Alger ya Algeria nazo zikitoa ofa ambazo zilikuwa ndogo kulinganisha na ile ya Wamorocco waliorudi kwa mara ya pili.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa ofa zimekuwa zinaingia na kuongeza dau, lakini hakuna uamuzi wowote kwa sasa wa kumuuza mchezaji huyo chipukizi.

“Licha ya ofa hizo nzito kutua Yanga, lakini viongozi wa klabu hiyo hawajafanyia kazi yoyote kati ya hizo, kwa vile ni mchezaji anayetegemewa kwa sasa na benchi halipo tayari kumpoteza kirahisi,” chanzo hicho kilisema.

Miezi minne iliyopita kupitia Mwanaspoti liliripoti kuwa Yanga imemsainisha Mzize mkataba mpya kimyakimya unaomfanya aendelee kusalia ndani ya klabu hiyo kwa miaka miwili zaidi hadi  2027.

Mmoja wa vigogo wa Yanga aliwahi kukaririwa na Mwanaspoti akisema kuwa kama kuna timu inataka kweli huduma ya mshambuliaji huyo, basi kwa haraka hara inabidi itoe kiasi cha Dola 1 milioni (zaidi ya Sh2 bilioni) na kwamba watamruhusu haraka aondoke akaitumikie.

“Hatuna shida ya kuuza wachezaji. Hakuna aliyetarajia kama tungemuuza Fiston Mayele, lakini tulifanya biashara, hivyo hata Mzize anaweza kuuzwa kama tukiona kuna timu imefikia bei tunayotaka,”  alisema bosi huyo, lakini inaelezwa Wydad imeamua kuongeza mzigo tofauti na ofa ya awali, ila viongozi wameamua kula bati kwa sasa.

Wakati flani Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe aliwahi kuzungumza na wanahabari na kusema kuwa Wydad wamekuwa wakigonga hodi mara kwa mara Yanga ili kumtaka Mzize, lakini uongozi umeichunia.

“Leo naweka wazi kuwa timu yoyote itakayomtaka mshambuliaji wetu Mzize ilete bilioni 20 iwe ni Wydad au lah, na kama ikitokea itakayofanya hivyo tutampeleka, mechi ya mwisho dhidi ya Waarabu  akiwafunga thamani yake itapanda zaidi,” alisema Kamwe wakati akizungumza na chombo flani cha habari.

Mchezaji huyo aliyetokea katika timu ya vijana ya klabu hiyo amekuwa akiboresha rekodi zake tangu aanze kuitumikia timu ya wakubwa, kwani msimu wa kwanza alimaliza akiwa na mabao matano, huku ule wa pili akifunga sita, lakini huu wa sasa amepindua meza mapema kwani raundi ya kwanza ya msimu amefunga mabao sita akiifikia rekodi ya uliopita.

Hata hivyo, kimataifa nako hajambo, kwani katika mechi tano ilizocheza Yanga hatua ya makundi, amecheza tatu sawa na dakika 225 akifunga mabao mawili dhidi ya TP Mazembe ambao walichezea kichapo cha mabao 3-1, mbali na mabao matatu aliyofunga katika mechi za awali za michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 

Katika msimu uliopita mchezaji huyo alinyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFA) kwa kufunga mabao matano yaliyoiwezesha Yanga kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo kwenye mashindano hayo.

Related Posts