Utafiti kubainisha uadilifu watendaji ZRA

Unguja. Wakati watendaji wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) wakitakiwa kuzingatia na kuyaishi maadili katika utendaji kazi wa kila siku, mamlaka hiyo inatarajia kufanya utafiti kubaini kiwango cha uadilifu kwa watumishi wake.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Mipango kutoka ZRA, Ahmed Haji Saadat, leo Januari 18, 2025 alipofungua mafunzo ya uadilifu katika ukusanyaji wa mapato kwa wafanyakazi wa mkoa wa kikodi Kaskazini Unguja yaliotolewa na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca).

“Idara inatarajia kufanya utafiti kupitia mkakati wake wa tano kwa mwaka ujao katika suala la maadili ili kuona hali ya maadili kwenye mamlaka,” amesema.

Amesema lazima wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utumishi wa umma ili kujiepusha na makosa yanayoweza kuepukika ikiwemo uhujumu uchumi na rushwa.

Ahmed amesema hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi kama hawazijui kanuni na miongozo, kwani ndiyo nguzo za kujenga maadili katika utendaji wao wa kila siku.

Mkuu wa kitengo cha maadili ya wafanyakazi wa ZRA, Khamis Ramadhan Khamis amewataka kutotoa siri za taasisi.

Amesema ZRA ina mkakati wa kupambana na rushwa pamoja na nyenzo nyingine zinazosimamia maadili ya wafanyakazi.

Khamis amesema ZRA imeunda kamati ya usimamizi wa maadili na imeshaanza kufanya kazi, hivyo aliwasisitiza wafanyakazi kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu na uwajibikaji.

Amesema ifahamike kuwa maadili siyo wizi pekee bali jambo hilo linaingia kwenye nidhamu, uadilifu, kuheshimu viongozi na wafanyakazi lakini pia wafanyabiashara ambao ndio walipakodi.

Meneja wa ZRA, mkoa wa kikodi Kaskazini Unguja, Hanii Moh’d Khamis, amesema lengo la mafunzo hayo ni kukuza maadili ya wafanyakazi.

Amebainisha kuwa ZRA ina jukumu kubwa la kuisaidia Serikali kukusanya mapato na kuiwezesha kutimiza malengo iliyojiwekea ya kufikisha maendeleo kwa wananchi.

“Tutambue kuwa tunapokusanya mapato basi tuna dhima kubwa kwa Mungu na Serikali hivyo tuendelee kufanya kazi kwa uadilifu na nidhamu,” amesema.

Kamanda Mkuu wa Zaeca, Ali Seif Ali amesema watazifikia taasisi zote kuzipatia elimu kwani mamlaka hiyo imeundwa kwa malengo makuu matatu, ikiwemo kufanya uchuguzi, kutoa elimu kwa umma juu ya elimu ya rushwa na kufanya udhibiti.

Amesema kuna changamoto za maadili katika taasisi nyingi za Serikali na binafsi na hayo yote ni kukosa uzalendo, kutokuwa na dhana za maadili na kutanguliza matamanio kuliko uzalendo wa nchi yao.

“Vijana wengi wamejenga dhana kwamba wakimaliza elimu ya juu na kutaka kufanya kazi katika taasisi za kifedha ikiwemo ZRA, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), BoT (Benki Kuu ya Tanzania) ili wawe na maisha mazuri bila ya kujua kwamba wameanza kuvunja maadili mapema,” amesema.

Amesema Zanzibar ipo nyuma katika maadili hivyo watahakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa watendaji serikalini na wananchi kwa ujumla ili kuona nchi inakuwa na watu wenye maadili na uzalendo.

Aliwapongeza viongozi wa ZRA kwa uamuzi wa kutoa elimu ili kuona watendaji wake wote katika taasisi hiyo wanasimamia suala la maadili na uadilifu katika utekekezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Related Posts