Wakulima Makiba walia kufungiwa maji, mazao kukauka

Arumeru. Baadhi ya wakulima wa mazao mbalimbali wa Kijiji cha Makiba Wilayani Arumeru, Mkoani Arusha, wamelalamikia kufungwa kwa mfereji wa maji ya kumwagilia mashamba yao na kusababisha mazao yao kukauka kwa ukame.

Wakulima zaidi ya 5,000 wameathirika na hali hiyo kutokana na ekari zao 1,000 za mazao mbalimbali ya mahindi na mbogamboga kukauka kutokana na kukosa maji ya kumwagilia.

Mmoja kati ya wakulima hao, Athanas Sumary akizungumza Januari 18 mwaka 2025, amesema hali ya wakulima wa eneo hilo la Makiba ni mbaya kutokana na mazao yao kukauka.

Sumary amesema baadhi ya watu wenye nguvu kuliko wao wamefunga maji na kutumia kwa ajili ya mashamba makubwa na kusababisha mazao ya wakulima wa Makiba kuathirika.

“Hali ni ngumu kwelikweli kwa upande wetu wakulima kwani mazao yetu yamekauka na hatua zisipochukuliwa athari itakuwa kubwa na kuathirika kabisa,” amesema Sumary.

Mkulima mwingine Joseph Justo amesema wanajipanga kuandamana kwenda kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Arumeru ili kufikisha kilio chao cha kukatiwa maji.

Justo amesema baadhi ya wakulima wakubwa kwenye mashamba yaliyopo Doli wamesababisha kufunga mfereji unaotiririsha maji kwenye mashamba yao.

Mkulima mwingine Pius Mmassy amesema baadhi yao wamechukua mikopo kwenye baadhi ya mabenki na taasisi za fedha ila watashindwa kulipa kwa sababu mazao yao yamekufa kwa ukame.

“Tunaomba Serikali iingilie kati suala hili kwani wakulima tutakuwa masikini kutokana na mikopo tuliyoichukua tutashindwa kuilipa,” amesema.

Mwenyekiti wa mfereji wa maji wa eneo hilo, Elieza Kisaka amesema kuna kigogo mmoja wa idara ya umwagiliaji wa wilaya hiyo amesababisha maji yao yafungwe.

Kisaka amesema kigogo huyo amesababisha maji yanayotiririka kutoka mfereji wa Doli yanayofika hadi Makiba kukatwa na kusababisha taharuki hiyo.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makiba, Godlisten Lema amewapongeza wakulima hao kwa kudai haki zao kistaarabu kwa kufuata hatua zinazotakiwa bila kufanya uharibifu wowote.

Lema ameeleza kuwa suala hilo walilifikisha kwenye ofisi ya ofisa Tarafa ya Mbuguni kwa ajili ya kufuatilia na kuchukuliwa hatua zaidi kwa waliosababisha maji kufungwa.

Diwani wa Kata ya Makiba, Samson Laizer amesema ili kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi inabidi mapendekezo manne yaliyotolewa yafanyiwe kazi.

Laizer amesema lengo ni kuhakikisha mustakabali wa suala hilo unafanyika kwani mamlaka husika watasimamia hilo ili kupunguza ukame unaowakabili wakulima hao wa Makiba.

Related Posts