Licha ya kukiri ugeni wake hapa nchini, Kocha Mkuu wa KenGold, Vladislav Herić amesema uzoefu na uwezo alionao timu hiyo itabaki salama Ligi Kuu.
Amesema anafahamu presha ni kubwa na haitakuwa kazi nyepesi lakini ushirikiano wake katika benchi la ufundi kwa makocha alionao utainusuru timu hiyo.
Akizungumza leo Januari 18, 2025 baada ya kutambulishwa rasmi, kocha huyo raia wa Serbia amesema anaamini katika uwezo na uzoefu wake akieleza kuwa KenGold itabaki salama Ligi Kuu japokuwa haitakuwa kwenye nafasi ya ubingwa.
Amesema moja ya falsafa yake ni soka la kasi, ushindani na havumilii mchezaji asiye na nidhamu na kwamba alichowahi kufanya kwa timu kadhaa Afrika ya Kusini atakionesha Tanzania.
“Nimefanya kazi Orlando Pirates, Chippa United, Marterbarg United, Black Leopard na kabla ya kuja hapa nilikuwa kituo cha michezo Welcome Football Afrika Kusini,” amesema na kuongeza.
“Ni mara ya kwanza kuja Tanzania lakini nimekuwa nafuatilia mtandaoni ‘YouTube’ mechi za Ligi ya Mabingwa na Shirikisho Afrika kwa Simba na Yanga, ila hilo siyo tatizo, tukutane uwanjani Jumatatu.”
Kocha huyo anayeonekana muongeaji sana, ameongeza kuwa pamoja na kukuta dirisha dogo la usajili limefungwa lakini baadhi ya nyota waliosaini kikosini humo amewahi kuwasikia na wengine kuwaona akieleza kuwa mashabiki wawe na matumaini.
“Ndio naisaka rekodi kwa mara ya kwanza hapa Tanzania, nitaanza kutengeneza timu kuanzia Jumatatu mazoezini kuona kikosi kitakuwaje,” amesema kocha huyo.
KenGold ambayo katika msimamo wa Ligi Kuu Bara inashika nafasi ya mwisho ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi 16, mbali na kumshusha kocha mpya pia kipindi cha usajili wa dirisha dogo kilichofunguliwa Desemba 15, 2024 na kufungwa Januari 15, 2025 imesajili wachezaji 22.
Wachezaji waliosaini na wanaotarajia kuiongoza timu hiyo ni kipa Mohamed Yusuph aliyetokea Dodoma Jiji, Bernard Morrison ‘BM3’ aliyetamba na Simba na Yanga, Obrey Chirwa, Zawadi Mauya na Emmanuel Asante.
Wamo pia Mubashid Seidu (Ghana), Kyala Lassa (Zambia), Elnest Kwofie (Ghana), Kelvin Yondan, Mathias Juvilian, Nassir Bofu, Abdul Abdulai, Thompson Unachi (Nigeria) na Maulid Mbegu.
Wengine ni Sele Bwenzi, Joseph Ambokege, Ahmed Chambela, Sadala Lipangile, Sandale Komanje, Rogers Gabriel, Fredrick Kalubunga na Erick Kabamba aliyetokea Vipers FC.